Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lwakatare awaita bungeni wabunge Chadema walioingia mitini
Habari za SiasaTangulizi

Lwakatare awaita bungeni wabunge Chadema walioingia mitini

Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini
Spread the love

WILFRED Lwakatare, kiongozi wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, waliorejea bungeni kupinga maelekezo ya viongozi wao ya kutoingia bungeni, amewaomba wenzake waliosalia nje, kurejea bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Jumamosi tarehe 9 Mei 2020, Lwakatare amesema, “ni vema wabunge wenzake, waliopo nje kurejea ndani ya Bunge, ili kumalizia kazi inayoelekea mwisho.”

“Hili ndio Bunge la mwisho la miaka mitano ya ubunge wetu. Nasi tumechaguliwa na wananchi kuja hapa kuwakilisha. Ni vema tukamalizia kazi hiyo,” ameeleza Lwakatare ambaye ni mbunge wa Bukoba Mjini mkoani Kagera

Lwakatare ametoa kauli hiyo kipindi ambacho baadhi ya wabunge wa Chadema wanaendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho tarehe 1 Mei 2020 ya kukaa karantini kwa siku 14.

Mbowe alitoa maagizo hayo baada ya kutokea kwa vifo vya wabunge na Watanzania aliodai vinatokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-14) hivyo kuwataka kujitenga kwa kipindi hicho ili kuangalia kama wana maambukizi au la.

Hata hivyo, maagizo hayo ya Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upizania Bungeni (KUB) yamepingwa na baadhi ya wabunge walioamua kushiriki shughuli za Bunge la bajeti linaloendelea Dodoma akiwamo Lwakatare.

Katika mazungumzo yake na waandishi leo Jumamosi, Lwakatare amesema maamuzi ya kutoingia bungeni, yaliamriwa na Mbowe na Ester Bulaya, mbunge wa Bunda Mjini na Mnadhimu wa Kambi ya upinzani bungeni, bila kuwashirikisha wenzao.

“Ule haukuwa uwamuzi wa pamoja. Ulikuwa uwamuzi wa watu wachache sana, wakiongozwa na Bulaya,” ameeleza Lwakatare na kuongeza, “hatuwezi kuwa na chama chenye mafanikio, ikiwa maamuzi yetu yanafanywa na kikundi cha watu wachache.”

Amesema, kutokana na maamuzi hayo kufanyika kienyeji, ndio maana kuna kundi kubwa la wabunge wa Chadema, wameamua kurejea bungeni. Na wengine wanaendelea kulalamikia uamuzi wa kuwazuia kurejea.

Amesema, mpaka sasa, kuna wabunge 16 wa Chadema wameshaingia bungeni. Amewataja waliongia bungeni jana, ni pamoja na Mbunge wa Karatu, William Qumbaro.

Amesema, kuna wabunge wamefika bungeni, lakini baadhi yao hawajaingia ndani ya Bunge, badala yake wameishia kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.

“Wengine wako lockdown, lakini wanaingia kwenye viunga vya Bunge kwa ajili ya kusaini mahudhurio na kupata posho. Baadhi yao, naambiwa wamenunua mabaibui ili wasiweze kutambulika,” amefafanua.

Lwakatare amesema, suala la kuingia bungeni siyo lake, bali ni makubaliano ya pamoja na wabunge wenzake, ambao walikutana na kutafakari utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wenzake.

Akizungumzia wabunge waliopo nje ya Dodoma, Lwakatare amesema, nao wamevunja maelekezo ya chama kwa kuwa chama kilielekeza wabunge wake wote, wabaki Dodoma.

Amesema, “kuna wenzetu wengine, kama vile Sugu (Joseph Mbilinyi), Lema (Godblless Lema, Halima Mdee na Mchungaji Peter Msigwa, hawako Dodoma, wakati maelekezo ya chama ni kwamba sote tubaki Dodoma. Hivyo kama sisi ni wasaliti, basi hawa nao ni wasaliti.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!