Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lwakatare ‘amrithi’ Mbowe U-KUB
Habari za Siasa

Lwakatare ‘amrithi’ Mbowe U-KUB

Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini
Spread the love

WILFRED Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini kupia Chadema, amekana kumpindua Freeman Mbowe, katika nafasi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), bali amechaguliwa na wabunge wenzake kushika nafasi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hivi karibuni wabunge 12 wa Chadema walimchagua Lwakatare kuwa KUB katika kipindi ambacho Mbowe na wabunge wengine wa chama hicho wanaendelea kuwa karantini kwa siku 14 ili kuangalia afya zao kama wana maambukizi ya virusi vya corona au la.

Wabunge hao walianza kukaa karantini tangu tarehe 1 Mei 2020 baada ya Mbowe kutangaza uamuzi huo kutokana na lofo cha mbunge wa Viti maalum, Mchungaji Getrude Rwakatare.

Pia, wabunge wengine waliofariki ni; mbunge wa viti maalum (CCM), Richard Ndassa, Sumve kupitia CCM na Balozi Augustine Mahiga ambaye alikuwa waziri wa katiba na sharia.

Hata hivyo, wabunge 12 wa Chadema hawakukubaliana na maagizo hayo ya Chadema yaliyotolewa na Mbowe na kuamua kuendelea na shughuli za Bunge huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwaonya wabunge hao ambao wamejiweka karantini.

Spika Ndugai alisema kitendo cha kutoonekana bungeni kwa siku 14 kinaweza kutafasiriwa kama utoro hivyo wanafikiria kuwakata mshahara wao.

Baadhi ya wabunge hao 12 walioingia bungeni ikiwamo Lwakatare ni, Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, David Silinde (Momba), Anthony Komu (Moshi Vijijini), Jaffari Michale (Moshi Mjini) na Joseph Selasini wa Rombo.

Wengine ni wa viti maalum; Joyce Sokombi, Mariaum Msabaha, Susan Masele, Latifa Chande na Subrina Sungura.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Ijumaa tarehe 8 Mei 2020, Lwakatare amesema wabunge hao walimchagua kuwa KUB, baada ya kushauriwa kuunda uongozi wao, kwa lengo la kurahisisha shughuli zao wakiwa bungeni.

Amedai hakuna mapinduzi yoyote yaliyofanyika, isipokuwa walichukua hatua hiyo ili kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao bungeni hapo, bila vikwazo.

“Usiku wa kuanzia jana mpaka leo sijalala kwa sababu nilijiruhusu mwenyewe kwamba simu iwe wazi nimpokee kila anayenipigia na kujibu kila anayenihoji. Kwa hiyo nimepata simu toka Tanzania nzima hususan mkoani kwangu, wakiwa na taharuki ya kusema Lwakatare amefanya mapinduzi ya kupata U-KUB, “ amesema Lwakatare

“Niseme mpaka dakika hii nashangaa huyo aliyeanzisha madhumuni yake ni yapi, lakini ukweli wenyewe, hakuna mapinduzi yeyote, suala lililofanyika na wenzangu walioko humu ni kwamba tulitaka tusikae humu kama kuku wa kienyeji.”

“Tukashauriwa miongoni mwetu wawepo watu wa kupokea majina kutoka upande wetu na kuwasilisha mezani,  ili kiti na meza iweze kupanga sawa sawa,” amesema Lwakatare ambaye tayari amekwisha kusema hatogombea tena ubunge

Lwakatare amesema bado wabunge hao wanaheshimu viongozi wa chama chao, isipokuwa hawakubaliani na maamuzi yao ya kutohudhuria vikao vya bunge.

“Viongozi wetu tunawaheshimu kwelikweli na tunawapenda lakini katika masuala mengine, unaangalia masuala ya kitaifa, ya chama chako na ufahamu wako. Na hii shule nilipigwa mwaka 2000 katika bunge la Pius Msekwa, kwa hiyo niliiva na naitambua hilo,” amesema Lwakatare.

Wakati huo huo, Lwakatare amesema hayuko tayari kuwa mtumwa wa nafsi kwa kuwa mnafki kile ambacho hakiamini, ndiyo maana anasimamia anachokiamini.

“Na mara nyingi na watu wanaanijua mimi napenda kusimamia nafsi yangu na sitaki kuwa mtumwa wa nafsi na nitaendelea kuwa hivyo. Na ndio maana pamoja na kwamba imebaki wiki chache, mimi nilishaaga,  sikutaka kutoka kwenye Bunge hili nikiwa mnafiki kwa kuamini nisichokiamini,” amesema Lwakatare.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!