Spread the love

 

SHAHIDI wa 12 wa Jamhuri, Luteni Denis Urio, amedai mashtaka ya ugaidi yanayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, sio ya kutungwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar ea Salaam…(endelea).

Luteni Urio ambaye ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ametoa madai hayo leo Jumatatu, tarehe 31 Januari 2022, akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbowe na wenzake watatu waliokuwa makomando wa JWTZ, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi Na. 16/2021, yenye mashtaka sita ya ugaidi.

Wakili Kibatala alimhoji Luteni Urio kwa nini wasiamini kuwa mashtaka hayo yalitungwa, baada ya shahidi huyo kudai aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa  Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Boaz, hakumpa ufafanuzi wa kwa nini maelezo yake ya ushahidi yalichelewa kuchukuliwa  baada ya kuripoti kwake mipango ya Mbowe kutaka kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Luteni Urio, alimripoti Mbowe kwa DCI Boaz Julai 2020 na kwamba maelezo yake yalichukuliwa na Askari Polisi aliyetajwa kwa jina la Inspekta Swilla, tarehe 11 Agosti 2020.

Inadaiwa kuwa, Luteni Urio alimripoti Mbowe kwa DCI Boaz kisha mkurugenzi huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai kumpanga aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Arusha (RCO), ACP Ramadhan Kingai, kufuatilia suala hilo baada ya mwanasiasa huyo kumuomba amtafutie makomando wa kutekeleza njama za vitendo vya kigaidi.

Mahojiano kati ya Wakili Kibatala na Luteni Urio yalikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Kwa kuwa wewe ndio mtoa taarifa tukiamini tuhuma zilitungwa kwanza  watu wa kushtakiwa wakatafutwa baadae, tutakuwa tumekosea nini?

Shahidi: Utakuwa umekosea

Wakati huo huo, Wakili Kibatala alimuuliza Luteni Urio, kwa nini Mbowe hakuwashirikisha watu anaowafahamu jeshini kupanga njama hizo badala yake alimtafuta yeye, ambapo mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Mbowe alikuwa na kaka yake wa  damu mwenye cheo kikubwa cha Jenerali, kiasi kwamba katika msiba wake Rais John Magufuli alikwenda na akampa pole Mbowe kwa kifo cha huyo jenerali, unafahamu ?

Shahidi: Nilisikia

Kibatala: Unasema akamuacha ndugu yake wa damu akakutafuta wewe mtu baki msaidiane kutekeleza ugaidi?

Shahidi: Sijui mimi, muulize yeye

Kibatala: Aliacha kupanga mipango na ndugu yake wa damu akakutafuta wewe Luteni?

Shahidi: Alishastaafu

Kibatala: Kati ya jenerali na wewe luteni nani anafahamu watu wengi jeshini?

Shahidi: Jenerali anajua

Wakati huo huo, Wakili Kibatala alimuuliza Luteni Urio kama kuna mtu mwingine tofauti na yeye alikuwa anatoa siri kwa ACP Kingai, zilizopelekea wenzake Mbowe, Ling’wenya na Kasekwa, kukamatwa tarehe 5 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kibatala: Kulikuwa kuna msiri tarehe 4, 5 na 6 Agosti 2020, alikuwa anampa taarifa Kingai kiasi kwamba tarehe  5 Agosti 2020 alimsimulia jinsi Adam, Ling’wenya na Moses Lijenje walivyovaa, swali la kwanza, huyo msiri alikuwa ni wewe au mwingine?

Shahidi: Sikuwa mimi, zaidi ya kutoa taarifa tu

Kibatala: DCI Boaz, ACP Kingai na pengine Inspekta Swilla waliwahi kukwambia kuna msiri wao mwingine zaidi yako wewe?

Shahidi: Hawajawahi kuniambia

Kibatala: Kulikuwa na mtu mwingine alikuwa ana acces kwa hawa vijana wawili na Moses ?

Shahidi: Sababu walikuwa wanafanya upelelezi …

Kibatala: Uliwahi kufahamu kama kuna mtu mwingine ambaye alikuwa anawafahamu?

Shahidi: Nishajibu mimi sifahamu

Kibatala:  Je unafahamu Rau Madukani walipokamatwa walikuwa wanafanya nini hasa pale?

Shahidi: Wala sifahamu kama walikamatiwa Rau Madukani

Kibatala: Kwa kuwa hawa walikuwa vijana wako umewatrain, unafahamu ama hufahamu kwamba Ling’wenya ana dada yake Asma anaishi Rau Madukani na kwamba walienda kusalimia?

Shahidi: hajawahi kuniambia

Kibatala: Ulivyoongea na Bwire uliulizia?

Shahidi: Sikumuulizia

Wakili Kibatala anaendelea kumhoji shahidi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *