Monday , 5 June 2023
Home Kitengo Maisha Elimu Lusako: Mateso UDSM hayatanirudisha nyuma
Elimu

Lusako: Mateso UDSM hayatanirudisha nyuma

Alphonce Lusako, Mwanafunzi aliyefukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Spread the love

KIJANA Alphonce Lusako amesema atapigania haki yake ya kusoma ndani ya ardhi ya Tanzania mpaka mwisho, licha ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kumfukuza kwa mara ya pili akiwa katika kipindi cha mitihani ya muhula wa kwanza wa masomo, anaandika Charles William.

Mara ya kwanza Lusako alifukuzwa na menejimenti ya UDSM mwaka 2011 kwa kuongoza mgomo wa kupinga wanafunzi wa mwaka wa kwanza kunyimwa mikopo ilihali kuna mikopo hewa inayotolewa na bodi ya mikopo. Amefukuzwa tena 26 Januri, mwaka huu baada ya kuanza upya masomo.

“Dhambi kubwa niyoitenda ndani ya taifa langu, ni kuongoza mgomo wa tarehe 11 Novemba 2011, ingawa siku moja baada ya mgomo huo wanafunzi wengi katika vyuo vikuu Tanzania walipewa mikopo tuliyoidai wakiwemo wanafunzi 144 wa UDSM. Sisi tulitolewa kafara.

“Wanafunzi 51 tulikamatwa na kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, tukashtakiwa kwa kufanya mkusanyiko bila kibali na kutotii amri halali ya polisi lakini tukashinda kesi hiyo. Tuliporudi chuo wanafunzi nane tukazuiliwa kuendelea na masomo,” amesema Lusako.

Akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Landmark, jijini Dar es Salaam, Lusako amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakikuwafukuza tu bali kiliishawishi Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ikatoa uamuzi wa kuwafuta wanafunzi hao katika mfumo wa elimu ya juu na kuzuia wasidahiliwe tena katika chuo chochote.

“Tumepigania haki yetu ya kusoma kwa njia mbalimbali ikiwemo kwenda mahakamani, lakini baadaye nikaifuta kesi hiyo ili tutatue mgogoro kidiplomasia. Nikaandika waraka kwenda kwa Rais (Jakaya Kikwete) na tukafanya vikao vitatu Ikulu ambavyo iliazimiwa turudishwe chuoni.

Lusako ameonesha barua iliyoandikwa na Prof. Yunus Mgaya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa TCU ambayo ilieleza uhalali wao wa kurejea masomoni kwa kuomba upya chuo ambayo ndiyo ilimfanya kijana huyo kuomba kudahiliwa katika vyuo vitatu tofauti mwaka 2016.

“Niliomba UDSM, Ardhi na IFM hata hivyo TCU wakanichagua niende kusoma UDSM, nikalipa ada na kusajiliwa. Cha kusikitisha nikiwa naanza mitihani yangu ya muhula wa kwanza menejimenti ya UDSM imeniondoa kwa hoja kuwa nilisajiliwa chuo hapo kimakosa na sistahili.

“Wananiambia niende TCU kama itaridhia nihamishiwe chuo kingine, lakini wanajua kuwa uhamisho hauwezi kuwa na maana kwa kuwa sina matokeo ya mitihani ya muhula ambayo naweza kuyahamishia chuo kingine, nimeiomba TCU iingilie kati na niruhusiwe kumalizia mitihani ili nihame lakini haijanijibu mpaka sasa,” amesema.

Lusako amesema kwamba hana kosa kubwa alilofanya kiasi cha kunyimwa haki ya kusoma, kwani madai yake katika mgomo wa mwaka 2011 yamedhihirika baada ya serikali ya awamu ya tano kubaini uwepo wa mikopo hewa na ufisadi katika bodi ya mikopo na kuwafukuza kazi watumishi wanaohusika.

“Ninataka kusoma, ndoto yangu ni kuwa mwanasheria ndani ya Tanzania. Nitaitimiza ndoto hii kwa kusoma, nitapambana kidiplomasia na ikishindikana nitaenda tena mahakamani. Hawapambani na mimi, wanapambana na elimu yangu ambao ndiyo nyenzo yangu pekee katika mapambano,” amesisitiza.

Alipoulizwa kuhusu mahali walipo wenzake nane aliofukuzwa nao UDSM na kufutwa katika mfumo wa elimu ya juu hapa nchini, Lusako amesema baadhi waliachana na mpango wa kurudi masomoni na kujikita katika shughuli zingine huku wengine wakipelekwa masomoni nje ya nchi na familia zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Elimu

Serikali yatoa Sh. 573 mil. kukamilisha wa ujenzi sekondari ulioanzishwa na wanakijiji

Spread the love  SERIKALI kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, imetenga Sh....

Elimu

CBE yaja na kozi mpya 16 zikiwemo za ujasiriamali na uvumbuzi

Spread the loveChuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuanzia mwaka wa masomo...

Elimu

SUA kuhakikisha tafiti zinazofanywa zisiachwe kwenye makabati

Spread the love  MRATIBU wa utafiti na machapisho katika kurugenzi ya uzamiri,...

Elimu

Watakaopata Division One St Anne Marie Academy kupewa iphone ya macho matatu

Spread the loveMkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy, Dk. Jasson...

error: Content is protected !!