June 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lukuvi: Watumishi ardhi wezi

Spread the love

WILLIAM Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kuwa, watumishi wengi katika idara ya ardhi nchini ni wezi, anaandika Moses Mseti.

Na kwamba, watumishi hao wamekuwa wakishirikiana na matajiri kunyanyasa wananchi wanyonge.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na wananchi walio na kero mbalimbali za ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Buhongwa ‘B’ Kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana, mkoani humo.

Lukuvi aliutumia mkutano huo kugawa hati kadhaa za nyumba za wananchi wa kata hiyo, huku akimuagiza mkuu wa mkoa huo, John Mongella na viongozi wengine kuhakikisha nyumba zaidi ya 3,5000 zilizo katika makazi holela zinapimwa, kupangwa na kutolewa hati kabla ya 30 Juni mwakani.

Amesema kuwa, makazi na viwanja vinavyokuwa vinapimwa na wataalamu wa ardhi, viwanja vingi wamekuwa wakijimilikisha wao wenyewe kitendo kinachosababisha kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi kila kukicha.

Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani mkoani Iringa amesema kuwa, wataalamu hao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya matajiri kuuza viwanja vya umma kwa manufaa yao binafsi kitendo ambacho alidai hatakubaliana nacho kukiona kikiendelea kujitokeza.

“Wataalamu hawa wanapoenda kupima shamba watakwambia viwanja vimetoka 10 lakini wao tayari wameishabaki na viwanja vyao vya kutosha na wakija wanakuonesha michoro na kukueleza maeneo mengi ni bondeni, milima na maeneo ya wazi.

“Ukiangalia zaidi ya asilimia 88 ya Watanzania hawana hati za nyumba na tumekuwa tukipoteza Sh. 1 trioni kwa mwaka kutokana na nyumba za Watanzania hao kutokuwa na hati za umiliki na kama wangekuwa na hati tungekusanya kodi kutoka kwao,” amesema Lukuvi.

Amesema kuwa, asilimia 82 ya Watanzania hususani wa mijini wamekuwa wakiishia kwa hofu ya nyumba zao kubomolewa na kwamba, umefika wakati wananchi wapimiwe viwanja vyao ili waweze kufahamu kama wapo katika eneo salama huku akidai tatizo hilo linatokana na urasimu wa watumishi hao.

Hata hivyo amesema kuwa, kutokana na nyumba nyingi kuwa katika makazi holela, wizara yake imekuja na mpango mkakati wa miaka 10 kuanzia sasa wa kuhakikisha nyumba zote za mjini zinapimwa na kupatiwa hati ili serikali iweze kukusanya kodi na kuongeza pato la  taifa.

Mongella amesema kuwa, atahakikisha anasimamia suala la upimaji wa ardhi na nyumba zote zitakazo pimwa zinapatiwa hati ya umiliki ili wananchi waweze kuzitumia kukopa fedha katika taasisi za kifedha.

“Mkuu (Lukuvi) labda niseme tu, hiyo kazi ulionipa kwamba ifikapo Juni 30 mwakani nyumba hizo ziwe zimepatiwa hati na nyumba nyingine zipimwe mimi nasema 1 Januari ya mwaka mpya zoezi litakuwa limekamilika,” amesema Mongella huku watumishi wakiguna wakiashiria kupinga.

error: Content is protected !!