August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lukuvi awabana watumishi sekta ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi

Spread the love

SERIKALI imewaagiza Maofisa ardhi wa Manispaa ya Iringa pamoja na halmashauri zote nchini kufanya kazi kwa weledi pamoja na kutatua kero za wananchi badala ya kutumia njia za ujanja ujanja ambazo zinalenga kuwakandamiza wanyonge na hivyo kuleta migogoro isiyokuwa na maana, anaandika Mwandishi Wetu.

Agizo hilo limetolewa na  Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akizindua mpango mkakati wa miaka 20 (Master Plan)  wa mji wa Iringa kuwa Jiji.

Waziri Lukuvi amesema serikali imedhamiria kumaliza kero zinazotokana na watumishi wa sekta ya ardhi ambao wamekuwa siyo waadilifu kwa kufunga mtambo maalumu utakaowezesha utoaji huduma kuwa rahisi huku akiagiza utoaji wa hati miliki za viwanja usiozidi mwezi mmoja nchi nzima.

“Na mtu yeyote ambaye atakayeona kwamba amelipa kila kitu na amechukua mwezi mmoja, simu yangu ipo wazi muda wote anitumie ujumbe mfupi wa sms nitawashughulikia wahusika,”amesema Lukuvi
Katika hatua nyingine waziri huyo  aliwataka viongozi wanaosimamia mpango huo kushirikisha mamlaka zingine zinazotakiwa kutoa huduma za kijamii hususani Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

Awali akitoa taarifa juu ya mpango mkakati huo  mkurugenzi wa halmashauri ya Iringa Dk .William Mafwele amesema mpango huo unalenga kubadili muonekano wa mji wa Iringa pamoja na kupanua wigo wa elimu na utalii jambo lililoungwa mkono na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe.

error: Content is protected !!