August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lukuvi ateua mchunguzi migogoro ya ardhi 

Spread the love

WILLIAM Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amemteua Jacob Mwambegele, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Biashara kuwa mchunguzi wa mgogoro sugu wa ardhi katika Vijiji vya Mabwegele na Kambaya, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza wakati akimkabidhi Jaji Mwambegele ripoti ya Kamati ya Usuluhishi leo jijini Dar es Salaam, Lukuvi amesema kuwa uamuzi huo wa kisheria umechukuliwa baada ya hatua ya awali ya usuluhishi kugonga mwamba.

“Awali nilimteua msuluhishi wa mgogoro huo, na baada ya hatua hiyo kushindikana,leo nimemteua mchunguzi kwa mujibu wa sheria ya ardhi kifungu namba 18 sura ya 113 na kifungu cha 7 (2) na (4) sura ya 114.

“Vifungu hivyo vinaruhusu Waziri kumteua Mchunguzi wa mgogoro wa ardhi ulioshindikana kusuluhishwa kwa njia ya usuluhishi na au ya utawala, na kwamba hatua ya mwisho inayofuata ni ya uchunguzi ambao unafanywa na mtu mwenye hadhi ya jaji katika mahakama kuu,”amesema Lukuvi

Lukuvi amesema kuwa amemteua Jaji Mwambegele pamoja na kamati ya watu 8 ambao watafanya uchunguzi kwa muda wa siku 60 ili kujua chanzo cha mgogoro huo uliodumu na kusumbua vichwa vya uongozi wa mkoa wa Morogoro na wizara kwa ujumla.

Amesema hatua hii ni mara ya kwanza kufanywa na serikali na kwamba lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha migogoro sugu ya ardhi inaisha Morogoro na katika mikoa yote nchini.

“Kijiji cha Mabwegele na kambaya ndivyo vilivyosababisha mgogoro wa ardhi ndani ya vijiji saba vilivyomo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro,”.

“Jaji Mwambegele baada ya kuwasili Morogoro, Kebwe Stephen Kebwe,Mkuu wa Mkoa huo, atamtambulisha kwa wanakijiji hao ili waweze kumpa ushirikiano wa kutosha,”amesema.

Amevitaja vijiji hivyo vilivyoathiriwa na mgogoro huo ikiwemo vijiji vya Dumira, Makongoro na Namfuni.

Lukuvi ametaja mambo kumi yatakayofanyiwa uchunguzi ikiwemo uhalali wa kisheria wa uanzishwaji wa kijiji cha Mabwegele, uzingatiwaji wa upimwaji wa ardhi kabla ya kuanzishwa, kuchuguzwa iwapo ardhi ya kijiji hicho kinatosheleza mahitaji ya wanakijiji hicho ikiwemo wafugaji.

“Pia itachunguzwa kwa nini baadhi ya viongozi wa vijiji hivyo walishindwa kutoa ushirikiano katika kamati ya usuluhishi jambo ambalo lilikwamisha utatuzi wa mgogoro huo,” amesema.

Hata hivyo Kebwe amesema kuwa, hatua hiyo itakuwa mwarobaini kwa mgogoro huo ambao ulidumu kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya vifo vya wakazi wa vijiji hivyo, uharibifu wa mazao na mifugo.

“Nashukuru kwa ushirikiano wa Waziri Lukuvi aliouonesha kwa kuwa ni mwarobaini wa mgogoro huo, na ninakuhakikishia nitatoa ushirikiano ili kutengeneza mazingira wezeshi,” amesema Kabwe.

 

error: Content is protected !!