August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lukuvi achemsha kuwapora ardhi matajiri

William Lukuvi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Spread the love

WILLIAM Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amekiri kuwa kuwanyang’anya mashamba matajiri waliogoma kuyaendeleza si jambo jepesi na kwamba mpaka sasa limemshinda, anaandika Dany Tibason.

Lukuvi amesema kuwa serikali imeshindwa kuyafutia hati miliki mashamba pori mengi ambayo hayajaendelezwa na wamiliki wake baada ya kubaini kuwa yamewekwa kama dhamana ya mabilioni ya fedha yaliyokopwa katika taasisi za kibenki hapa nchini.

“Mikopo yote iliyokopwa benki kupitia mashamba hayo, imesajiliwa kwa msajili hivyo hatuwezi kukurupuka, lazima tufuate sheria katika kufuta mashamba hayo ili tusije kuingia kwenye matatizo na kubaki tukijilaumu.

Kuna shamba moja limekopewa Dola za kimarekani 16 milioni mara nane, hapo utaona jinsi ilivyo hatari kulifutia hati yake na kulirejeshwa kwa umma kwani unaweza kuingia katika mgogoro mkubwa na taasisi hizo za kifedha,” amesema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alikuwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, baada ya serikali kuwasilisha taarifa ya ardhi kuhusu hatma ya utaifishaji wa mashamba makubwa yaliyotelekezwa.

“Tunazitahadharisha taasisi za kibenki nchini, ziwe makini katika utoaji mikopo kwani endapo itatoa mkopo kwa dhamana ya shamba, kuna uwezekano wa kutokea kwa migogoro mikubwa kwani wamiliki huyatumia kukopa fedha katika taasisi tofauti za kifedha,” ameonya.

Lukuvi amesema kuwa serikali iataendelea kupambana na wote wanaomiliki mashamba makubwa bila kuyaendeleza na kusisitiza kuwa ardhi yote ni mali ya Rais wa Tanzaniana ni jukumu la serikali kulinda umiliki na matumizi halali.

“Rais amenipa jukumu la kuhakikisha nafuta mashamba yote yasiyoendelezwa na kazi hiyo inaendelea lakini tunahakikisha kuwa tunafuata sheria ili tusije tukashitakiwa,” amesema.

error: Content is protected !!