July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lukuvi aipa siku 10 kamati ya ardhi

Spread the love

WILLIAM Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametoa siku 10 kwa kamati ya ardhi kutoa maelezo namna watakavyotatua mgogoro wa nyumba kwa wakazi wa Magomeni Kota (Magomeni Hospitali) dhidi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, anaandika Hamisi Mguta.

Lukuvi ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake wakati akisikiliza malalamiko ya waliokua wakazi wa kota hizo wapatao 644 wakitaka eneo hilo lisiwe chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Nyumba hizo zilizobomolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni tangu mwaka 2011 ambapo wakazi hao walitakiwa kuondoka kwa makubaliano ya kupisha ujenzi wa nyumba mpya zilizoelezwa kuwa ni za bei nafuu.

Amesema, nyumba hizo zilikua chini ya serikali na ndio iliyoamua kuzipa halmashauri hivyo kwa kuwa serikali ya sasa haihitaji kulaza mambo, kamati hiyo ikiwa ni moja ya chombo cha ushauri itatakiwa kuwasilisha namna watu hao watakavyotekelezewa ombi lao.

“Kazi yetu ni kunyoosha yaliyopinda, kuwafuta machozi watu wote wanaolia na nitamuomba Mh, Waziri Mkuu nisiende Dodoma kwa ajili ya kulishughulikia hili,” amesema.

George Abel, Mwenyekiti wa Kamati ya wanakota hao amesema, kwa kuwa Halmashauri ya Kinondoni inaonekana kushindwa walichokiahidi, waziri aongee na rais ili eneo hilo liwe chini ya wizara.

Amesema, kwa kuwa ardhi ipo chini ya rais hivyo abadilishe eneo liwe chini ya wizara na zijengwe nyumba na wapo tayari kupanga kwa bei yoyote.

“Tulipeleka kesi mahakamani na halmashauri ilituomba tutoke nje ya mahakama ili tukubaliane kupisha ujenzi na baadaye tuwe wapangaji, wanunuzi na ndio maana huko tunapoishi walikua wanatulipia kodi,”amesema.

Rukia Mwene, mwanakamati aliyehudhuria kikao hicho amesema, malalamiko hayo yamedumu kwa miaka mitano huku mateso yakiendelea.

“Wapo wanakota wengine wengi hawajafika hapa kwa sababu ni watu wazee hivyo tunakuomba waziri utusaidie ili tupate makazi tulivu kama zamani,” amesema.

error: Content is protected !!