January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Luku zataabisha wateja TANESCO

Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud

Spread the love

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), limeshindwa kutoa huduma kwa wateja wake wanaotumia meta za LUKU kutokana na hitilafu iliyojitokeza katika mtambo wa kuuza vocha tangu Februari 27 mwaka huu. Anaandika Deusdedit Jovin…(endelea).

Tangu Ijumaa ya Februari 27, wateja wa TANESCO wamekuwa wakihaha kutafuta huduma ya LUKU bila mafanikio. Kuna matatizo ya aina tatu yameripotiwa na wateja wa TANESCO mpaka sasa.

Baadhi ya wateja waliojaribu kununua vocha kupitia kwa mawakala wa TANESCO walishindwa kupata huduma kwa kuwa mfumo ulikuwa hautoi majibu.

Wateja wengine walifanikiwa kununua vocha za LUKU kupitia simu zao za mikononi, lakini vocha hizo zikakataliwa na mita za TANESCO zilizosimikwa majumbani mwao.

Pia, kuna wateja waliojaribu kununua vocha za LUKU kupitia simu zao za mikononi lakini pesa ikakatwa bilakupatiwa vocha yoyote ya LUKU.

Kwa siku zote hizo hakuna taarifa iliyotolewa kwa umma kueleza tatizo lililopo,- hali ambayo iliwafanya baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri kulizana masawali yasiyo na majibu wakati wakiwa kwenye hafla ya kuaga mwili wa hayati Kapteni John Komba.

Msemaji wa TANESCO, Adrian Severin, alipoulizwa na MwanaHALISI Online kuhusu tatizo lililopo, alisema kuwa mfumo wao wa kompyuta unaotumika kuuza vocha za LUKU una matatizo tangu Ijumaa ya Februari 27.

“Ni kweli mfumo wetu wa kompyuta una matatizo. Tayari mafundi kutoka Afrika Kusini wako kazini kunusuru hali,” amesema.

Severin alieleza kwamba, mara baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wateja walifanya jitihada za kumtaarifu mtaalam aliyewauzia mfumo huu kwa ajili ya matengenezo. Mtaalam huyo alithibitisha kwamba mtambo ulikuwa na matatizo makubwa.

Alisema kwamba, mpaka Jumapili matengenezo hayo yalikuwa yanaendelea yakiwa yametatua nusu ya tatizo.

“Mafundi walifanikiwa kuuwezesha mtambo kuzalisha vocha kwa wateja wanaojaribu kununua kwa njia ya simu lakini vocha hizo zikakataliwa na mita za TANESCO,” alieleza.

Alipoulizwa kuhusu hatua walizochukua mafundi baada ya tatizo hilo jipya, alisema, “baada ya kupata taarifa hii mpya mafundi waliuzima kabisa mtambo ili kupata fursa ya kuuimarisha zaidi. Mpaka leo (Jumatatu) mafundi wako katika matengenezo.”

Alipotakiwa aseme ni lini wateja wa TANESCO watarajie huduma za LUKU kurejea katika hali yake ya kawaida, alisema, “tunatarajia kwamba kufikia leo (jana) jioni wataalam wetu watakuwa wamemaliza matatizo haya.”

Alipotakiwa asema ni kitu gani wafanye wateja ambao tayari wamekatwa fedha zao bila kupata vocha za LUKU alieleza, “Wateja wote waliokatwa fedha zao watafidiwa. Watunze risiti zao halafu waje nazo ofisini.”

MwanaHALISI Online ilipotaka kufahamu kwanini matatizo haya yamedumu kwa siku nne mfululizo bila kupatiwa ufumbuzi, amesema sababu kubwa ni ukweli kwamba sehemu ya mtambo wa LUKU imesimikwa nje ya nchi huko Afrika Kusini.

Alipoulizwa aseme kama TANESCO wanao mfumo kwa ajili ya matumizi ya dharula pale mfumo wa kawaida unapokuwa na hitilafu alisema, “security modules (program za kulinda usalama wa kompyuta) tulizo nazo hazina nakala ya dharula kwa hapa Tanzania”.

Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, alipotafutwa ili aeleze ni kwa nini wizara iliiruhusu TANESCO kununua mtambo wa malipo ya LUKU nje ya nchi na kuacha usimikwe huko alikuwa mkali.

“Sisi wizarani tunatengeza sera tu. Mambo ya utendaji walize TANESCO,” alitamka kwa ukali.

Alipoambiwa kwamba uamuzi wa kutafuta huduma nje ya nchi na namna ya kuendesha huduma vinaongozwa na sera za wizara, alisema “hakuna mtambo uliosimikwa nje ya nchi. Nenda pale Ubungo Makao Makuu ya TANESCO utaukuta mtambo wa LUKU kwenye server room (chumba cha kompyuta kubwa).”

Hata hivyo, hapo awali, msemaji wa TANESCO Adrina Severin aliliambia gazeti hili kwamba sehemu ya mitambo ya LUKU iko Afrika Kusini na kwamba wataalam wanaoendelea kutatua tatizo hili wako kule kule sasa hivi.

Mpaka tunakwenda mitamboni matatizo ya mtambo wa LUKU yalikuwa bado hayajapatiwa suluhisho.

error: Content is protected !!