Nyota wa Atletico Madrid, Luis Suarez amezidi kumfungulia mlango wa kutokea Kocha Mkuu wa Barcelona, Ronald Koeman baada ya kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi mnono wa bao 2-0.
Raia huyo wa Uruguay (34), alianza kwa kummegea pande safi kiungo matata wa Atletico, Thomas Lemar aliyeweka kambani bao la kwanza dakika ya 23 huku Suarez mwenyewe akishindilia msumari wa pili na wa mwisho dakika ya 44.
Mchezo huo uliopigwa jana tarehe 2 Oktoba 2021 katika uwanja wa Wanda Metropolitano, ulikuwa wa ligi kuu nchini Hispania maarufu kama La liga.
Gwiji huyo wa zamani wa Barcelona juhudi zake uwanjani zilitafsirika kuwa ni hasira baada ya kutemwa na klabu hiyo pamoja na mastaa wengine ili timu hiyo iweze kumudu kukabiliana na deni la zaidi ya paundi bilioni moja.
Hata hivyo, sasa hali inazidi kuwa mbaya ndani ya Barcelona ambayo tangu ligi hiyo ianze kwani imejikusanyia pointi 12 pekee katika michezo saba na kushika nafasi ya tisa ilihali Atletico ni wa pili wakiwa pinti 17 baada ya kushuka dimbani mara nane, Real Madrid ndio wanaoongoza ligi kwa pointi 17 baada ya kushuka uwanjani mara saba.
Pia fedheha zaidi kwa Barcelona inazidi kufuka moshi baada ya kupoteza michezo yake ya awali ya Klabu Bingwa barani Ulaya yaani Uefa Champions League.
Hata hivyo, baada ya mchezo wa jana Rais wa Barcelona, Joan Laporta amesisitiza kibarua cha kocha huyo bado kipo salama.
“Koeman ataendelea kuwa kocha wa Barca. Tunaelewa anapitia changamoto mbalimbali hivyo anastahili kuaminiwa,” amesema.
Suarez alilazimishwa kutoka Barcelona Septemba 2020 baada ya Koeman kumwambia hakuwa sehemu ya mipango yake.
Fowadi huyo mashuhuri aliendelea kufunga mabao 21 ndani ya La Liga na kuiwezesha Atletico kunyakua taji la ligi hiyo msimu uliopita.
Leave a comment