December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lugola, Polisi watoke mafichoni kujibu maswali haya  

Spread the love

TUKIO la dereva wa basi la daladala maarufu Hiace, Andrew Kiwia, limeibua maswali yasiyo na majibu hasa baada ya kauli ya kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah. Anaandika Mwandishi Maalum…(endelea).

Wakati maswali hayo yakiibuka, mama mzazi wa marehemu, Haikamesia Kimambo, jana alisisitiza kuwa hawatachukua mwili huo hadi taratibu za kisheria zitakapozingatiwa na mamlaka.

Taratibu hizo ni kufanyika uchunguzi wa kijinai ikiwamo uchunguzi huru wa mwili wa marehemu (postmortem), ili kubaini kiini cha kifo chake kwani wanaamini si cha kawaida.

Taarifa hii imeandikwa na Mwananchi digital, kwa umuhimu na unyeti wa suala hili hasa mauaji ya raia wasio na hatia mikononi mwa vyombo vya dola. Tumeyaleta ili kuyapeleka zaidi kwa Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pia Jeshi la Polisi kutoa majibu.

1.   Kama mtuhumiwa na mwenzake waliokuwa wakinyoana nywele walikamatwa na gongo, je polisi walijaza hati ya ukamataji (seizure note) ili kuchukua kidhibiti cha gongo kama kielelezo namna sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai (CPA) inavyotaka?

2. Kama polisi walimkamata mtuhumiwa na mwenzake kwa kumshuku ni mnywaji wa pombe haramu ya gongo, kwa nini hawakuchukua sampuli ya damu ili kuipeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali ili kuthibitisha tuhuma dhidi yao?

3. Kama kweli usiku wa Jumapili ya Septemba 23 mtuhumiwa huyo alionekana kama ana matatizo ya akili kwa kumwaga maji mahabusu, kwa nini polisi hawakumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi iliyopo mita 100 tu na yenye wodi ya vichaa?

4. Kama mtuhumiwa alirukwa na akili na kumwaga maji chumba cha mahabusu hadi wengine wakahamishiwa eneo lingine, ilikuaje mtu mwenye tatizo la akili akaachwa mwenyewe mahabusu kwenye chumba kilicholoa maji?

5. Kama mahabusu wenzake ndiyo waliotoa taarifa za mtuhumiwa huyo kujinyonga, je hao mahabusu waliwezaje kumuona wakati hawakuwa wote chumba kimoja?

6. Kama alijinyonga alfajiri ya Septemba 24, kwa nini aliondolewa kituoni kati ya saa 3:00 na 4:00 asubuhi ikiwa ni zaidi ya saa tano kupita tangu ajinyonge?

7. Kwa nini polisi waliwafukuza ndugu na jamaa waliokuwapo eneo la Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kwa ajili ya kuwapelekea watuhumiwa chai na kuwaombea dhamana, kisha polisi kuonekana wakimpakia mtu aliyeonekana kuzirai au asiyejitambua kwenye gari lao?

8. Kama alijinyonga kwa suruali ya jeans, makovu yanayoonekana katika paji la uso na mikononi yalitokana na nini?

9. Kama maelezo ya RPC ni ya kweli, inakuaje mahabusu aliyekuwa chumba kimoja na mtuhumiwa adai alipozinduka usiku wa manane wa Jumapili kuamkia Jumatatu ya Septemba 24 hakumuona mwenzake? Ni nani kati ya marehemu na mwenzake alihamishwa?

10. Kwa nini baada ya mtuhumiwa kufa Jumatatu ya Septemba 24, polisi hawakuijulisha familia hata baada ya mama mzazi kupeleka chakula mchana na polisi kumweleza mwanaye hayupo mahabusu?

error: Content is protected !!