Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lugola alikoroga tena, Bunge lamng’ang’ania
Habari za SiasaTangulizi

Lugola alikoroga tena, Bunge lamng’ang’ania

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Zuberi Kabwe, ameituhumu serikali kwa kile alichokiita, “kushindwa au kunyamazia,” vitendo vya ubakaji wanavyofanyiwa wapigakura wake. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, leo tarehe 21 Mei 2019, Zitto alisema, kwa miaka mitatu mfululizo sasa, ndani ya jimbo lake la uchaguzi, limezuka kundi la vijana, wanaovamia akina mama na kuwabaka.

Alisema, “…mheshimiwa mwenyekiti, katika jimbo langu la Kigoma Mjini, kumezuka tabia ya vijana kujipaka oil chafu na kuvamia wanawake hasa wajane na wale ambao hawana wapendwa kwenye maisha yao na kuwabaka.”

Akitumia Kanuni ya 47 (1), Zitto alisema, “usiku wa kuamkia jana (Jumatatu), mama mmoja ambaye siwezi kumtaja jina, amejeruhiwa kwa kupigwa nondo ya kichwa na mmoja wa hao vijana hao na sasa yuko hospitali. Mwingine amepigwa kisu na kujeruhiwa vibaya.”

Alisema, pamoja na kuwapo kwa matukio hayo na wahusika kuripoti kwenye vituo vya polisi, “lakini serikali imeshindwa kuchukua hatua za kukabiliana na watu hao.”

Alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu. Wakati huo, Bunge lilikuwa chini ya uenyekiti wa Najma Giga, mbunge wa Viti Maalum kutokea Zanzibar.

Akizungumza kwa uchungu, Zitto alisema, shirika lisilo la kiserikali la Tamasha, limekusanya takwimu kuhusu matukio 43 yanaohusu wanaume hao kubaka wanawake toka mwaka 2016.

Amesema, shirika hilo lilimwandikia barua yeye (Zitto) kama mbunge wa jimbo, waziri wa mambo ya ndani na taasisi mbalimbali ikiwamo Twaweza, ili kuwataarifu hali hiyo. Amesema, mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote katika kuzuia uhalifu huo.

“Nimelileta suala hili hapa bungeni, ili chombo hiki cha wananchi kiweze kufahamu na kuchukua hatua. Hili ni tukio la aibu kwa kweli, na mimi kama mbunge wa eneo hilo linanisononesha na kunisikitisha sana,” ameeleza.

Amesema, “ninaona aibu sana kwamba tunaweza tukashindwa kulinda dada zetu, mama zetu na watoto zetu.

“Ninaomba kiti, kielekeze serikali ilete ndani ya Bunge, taarifa ya hatua gani wamechukua mpaka sasa, kukomesha vitendo hivi na kuchukua hatua kali kwa wote wanaodhalilisha wanawake.”

Muda wote ambao Zitto alikuwa akitoa maelezo yake, Bunge lilikuwa kimya kumsikiliza na baadaye ndipo mwenyekiti Giga alitoa nafasi kwa serikali kutoa maelezo.

Akijibu madai hayo ya Zitto, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliliambia Bunge, kwamba jeshi la polisi halijapokea taarifa za kuwapo kwa vitendo hivyo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, kama ambavyo mbunge huyo amedai.

Alisema, “huo ni mchezo wa teleza” na kwamba tatizo hilo halina ukubwa unaoelezewa na Zitto.

Alisema, vitendo hivyo vilikuwapo siku za nyuma, lakini kwa sasa, tayari vimedhibitiwa na kwamba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliyopita, jeshi halijapokea taarifa ya kuwapo vitendo hivyo.

Amesema, kwa mujibu wa sheria, ubakaji ni kosa la jinai na kwamba ubakaji umekuwa ukitokea maeneo yote na si Kigoma pekee yake.

Amesema, “vitendo hivi, vilianzia mwaka 2014 ambapo akinamama wa mkoa wa Kigoma ambao ni wajane au ambao hawana wanaume au waume zao wamesafiri, walikuwa wanajikuta wako na mtu ambaye haonekani kwa macho na mwanamama anajikuta sehemu zake za siri zimelowa.

“Halafu anaponyanyuka anaona kama mtu anapotaka kumshika, yule mtu anateleza. Kwa hiyo, dhana ya udhalilishaji kwa mtindo wa teleza ulipoanzia na walikuwa wanaingia kwenye pembe ya nyumba.”

Katika maelezo yake, Lugola amedai kuwa suala hilo halina uzito ambao Zitto ameueleza.

“Mheshimiwa mwenyekiti, jambo hili siyo kubwa kama linayoelezwa na mheshimiwa Zitto.”

Amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja, hakuna tukio lolote mkoani Kigoma lililohusisha mwanamke kubakwa.

“Yapo matukio matatu ya kubakwa yanayohusisha wanawake kujeruhiwa katika nyumba zao. Lakini hayana uhusiano na haya anayoeleza Zitto,” ameeleza.

Akageukia taasisi binafsi zinazofanya tafiti kwa kusema, kuna baadhi ya taasisi au mtu mmoja mmoja, wanakuza mambo na kujenga hofu.

Alisema, “niseme bayana, taasisi ambazo zinakwenda kufanya tafiti na kukuza mambo, tumeanza kuziorodhesha na hatua zitaanza kuchukuliwa.”

Baada ya kauli hiyo, Zitto alisimama na kuomba kutoa taarifa ikiwa ni mara ya pili, lakini Giga alimzuia akimtaka kusubiri waziri Lugola amalize.

“Kama Zitto una taarifa hizo, niko tayari kwenda Kigoma na nitachukua hatua,” amesema Waziri Lugola.

Baada ya Lugola kumaliza, Giga alimpa nafasi Zitto ambaye alianza kwa kusema, “ni kwa bahati mbaya sana, waziri mwenye dhamana kwenye usalama wa wananchi wetu, wakiwemo wanawake kazungumza kama alivyozungumza sasa.

“Mwanzoni mwa mwaka 2016, akina mama hawa waliripoti polisi na kamanda aliyekuwepo alidhibiti na baadaye alihamishwa. Ma RPC waliofuata walianza kuwadhihaki na kuwaita wanawake wa teleza. Ni akina mama gani watakwenda polisi kutoa taarifa na kukejeliwa kisha akarudi,” amehoji Zitto.

Kutokana na kauli hiyo, Lugola alisimama kutaka kuzungumza, lakini Giga alimzuia akimwambia “mheshimi waziri tulia, mwache mheshimiwa Zitto azungumze.”

Ameongeza, “mimi kama mbunge wa Kigoma Mjini, ninawaomba wanawake wa ndani ya Bunge hili, wafumbe macho, kuvuta hisia za kuingiliwa waone ilivyoshida katika mambo hayo mabaya.”

Baada ya Zitto kumaliza kuhutubia, mwenyekiti Giga akasema, “waziri kama huna taarifa, hili jambo hata liwe dogo, litaleta shida. Suala la ubakaji liwe kwa watoto au wakubwa sio la kuvumiliwa.” Akaagiza waziri Lugola aende Kigoma kufuatilia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!