Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko LSF, NGO’s zajadili mfumo upatikanaji haki Tanzania
Habari Mchanganyiko

LSF, NGO’s zajadili mfumo upatikanaji haki Tanzania

Spread the love

 

SHIRIKA linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania, kupitia uwezeshaji wa kisheria (LSF), linaendesha mkutano wa siku mbili kwa ajili ya kujadili mfumo wa upatikanaji haki nchini humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mkutano huo unaofanyika kuanzia leo tarehe 23 hadi 24 Februari 2021, jijini Dar es Salaam, umekutanisha mashirika yasiyo ya serikali (NGO’s) 200, yanayitoa huduma ya msaada wa kisheria (Paralegals).

Akizungumza na washiriki wa mkutano huo uliofanyika kupitia njia ya mtandao, Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema, mkutano huo unafanyika kwa ajili ya kuweka mipango mkakati wa kufanya kazi kati ya LSF na wadau wake wote wa masusala ya haki na hasa mashirika ya wasaidizi wa kisheria katika kipindi hiki cha mwaka 2021.

“Nina furaha sana kuonana nanyi leo.  Ingawaje mko mbali lakini kupitia teknolojia tunaweza kukutana na kujadili maswala muhimu katika mustakabadhi mzima wa upatikanaji wa haki.  Nina furaha zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wadau wetu nyinyi mmefanya kazi kubwa sana na imetupa matokeo makubwa ukilinganisha na malengo tuliyokuwa tumejiwekea,” amesema Ng’wanakilala.

Ng’wanakilala amesema mkutano huo ni sehemu ya majukwaa mbalimbali ambayo LSF huandaa kila mwaka, ili kukutana na watendaji wakuu wa Paralegals, ikiwemo wakurugenzi wakuu wa mashirika na watendaji wengine wa mashirika haya ili kuangalia maeneo muhimu ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji haki nchini.

Ng’wanakilala amesema, mikutano hiyo inayoendeshwa kila mwaka na LSF kwa ajili ya kutathimini hali ya upatikanaji haki nchini, imeongeza chachu ya Paralalegals kuwafikia wananchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa LSF, ametoa mfano wa mkutano uliofanyika 2020, akisema kwamba uliwawezesha wadau wa LSF walifanikiwa kutoa elimu ya masuala ya kisheria kwa watu milioni 6.4, na kwamba asilimia 45 kati yao walikuwa wanaume na wanawake walikuwa asilimia 55.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu kazi zinazofanywa na wadau wetu.  Tunatumia taarifa hizi kwa ajili ya kupanga mikakati mizuri ili kuweza kuwafikia watu wengi hasa wenye uhitaji kama vile wanawake na watoto. Lengo letu ni kuleta maendeleo kwakuwa tunaamini kabisa hakuna maendeleo bila haki,” amefafanua Ng’wanakilala.

Aidha Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Bumbuli (BPO), mkoani Tanga, Ramadhani Ibrahimu Mtana, ameishukuru LSF kwa kazi kubwa ya kuendelea kutoa ruzuku kwa wadau wake na hasa wasaidizi wa kisheria kwa kuwa suala la fedha limekuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“LSF kama wadau wetu mkuu tunakushukuru sana kwani umekuwa mstari wa mbele kutoa mchango wako hasa ruzuku katika taasisi zetu. Kupitia ruzuku hizi tumeweza kuhudumia wananchi wengi nchini hasa wanawake ambao wanakumbana na changamoto mbalimbali kama vile kesi za mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na matatizo mengine,”  amesema Mtana.

Mkutano huo maalumu wa LSF kwa ajili ya kukutana na wadau wake  nchi nzima, pamoja na mashirika yanayotekeleza miradi ya upatikaji wa haki, unalenga  kujadili masuala ya kiutendaji katika suala zima la utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji hususani wanawake na watoto.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!