January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa yametimia, aitenga CCM

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) akimkabidhi kadi Waziri Mstaafu, Edward Lowassa alipotangaza kujiunga rasmi na chama hicho

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) akimkabidhi kadi Waziri Mstaafu, Edward Lowassa alipotangaza kujiunga rasmi na chama hicho

Spread the love

EDWARD Lowassa, amekuwa mwanasiasa wa kwanza nchini aliyefikia ngazi ya Waziri Mkuu katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuamua kukihama chama hicho alichokitumikia kwa miaka 30. Lowassa amehamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaandika Pendo Omary . …(endelea).

Lowassa amejiunga Chadema leo kwa kukabidhiwa kadi ya uanachama ya chama hicho katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Bahari Beach, nje kidogo ya jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na chama hicho na kushuhudiwa na wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ilishuhudiwa pia mkewe, Regina, naye akikabidhiwa kadi ya Chadema, ikiashiria kuwa naye amejitenga na CCM.

Katika hotuba yake iliyotangazwa sambamba na tukio zima hilo kwenye vyombo vya habari, Lowassa alisema ameachana na CCM kwa sababu amechoka kushuhudia uongozi unaoamini katika kusikiliza majungu, uongo, fitina, mizengwe na kuvunja katiba yake wenyewe.

Lowassa alisihi watu wote ndani ya CCM na Watanzania wengine wanaomuunga mkono, waangalie ukweli huo na kuungana naye kwenye upande wa kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa.

Waalikwa katika mkutano huo walianza kuingia ukumbini saa 9 mchana huku ulinzi ukiimarishwa kwa kukaguliwa na vifaa maalum na kuhakikiwa majina ya waalikwa. Lowassa alianza kuzungumza saa 10.31 alasiri baada ya kukaribishwa na Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.

Lowassa ambaye ni mbunge wa Monduli, Arusha akizungumza kabla ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Baada ya kutafakari kwa kina, nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chadema, kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu,” alisema.

Amesema “Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI! …tuyatafute mabadikilo nje ya CCM. CCM sio mama yangu.”

Lowassa amesema ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuhamia Chadema, baada ya mchakato wa kuteua wagombea wa nafasi ya urais ndani ya CCM kugubikwa na mizengwe, ukiukaji wa maadili, uvunjaji wa katiba na taratibu za uchaguzi.

Zaidi ya hayo, Lowassa amesema uchaguzi huo ulisimamiwa kwa upendeleo na chuki iliyokithiri dhidi yake. Kikatiba, alisema Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanachama wanaoomba kugombea urais kupitia chama hicho.

Lowassa alikuwa miongoni mwa makada 38 waliorudisha fomu za kusaka ridhaa ya CCM kugombea urais katika uchaguzi ujao. Jina lake ni miongoni mwa yale 33 ambayo haikujulikana kama yalifika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC).

Majina matano ya Bernard Membe, John Magufuli, January Makamba, Dk. Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali ndio walioingia Kamati Kuu.

“Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vilitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM,” amesema Lowassa.

Lowassa amesema wazi kuwa yaliyomkuta ni mpango wa muda mrefu ulioandaliwa pamoja na kujulikana pasina shaka kuwa yeye alikuwa mgombea aliyeongoza kwa kuungwa mkono kuliko wagombea wengine wote.

“Niliwekewa mizegwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote.

“Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu,” alisema katika maelezo yenye ufasaha kwa mara ya kwanza tangu vikao vya CCM vya maamuzi ya kutafuta mgombea wake wa urais kumalizika wiki mbili zilizopita.

Amesema kwa yaliyotokea Dodoma atakuwa mnafiki kama ataendelea kujidanganya yeye mwenyewe na umma wa Watanzania kuwa bado ana imani na CCM au kuwa “CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.”

Amesema, “CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.”

Akieleza kuhusu mikakati iliyoandaliwa na CCM ili kummaliza kisiasa hata kabla ya kura ya maoni, Lowassa alisema “…kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo usio na kifani.

“Nimeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu, uongozi wa CCM na Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.”

Lowassa akijibu maswali machache ya waandishi, alisema amechoka na kukerwa na tuhuma anazozushiwa kuhusu tuhuma kuwa alihusika na ufisadi wa mkataba wa kufua umeme ambapo kampuni ya Richmond ya Marekani ilipewa zabuni mwaka 2006.

“Nimechoka na Richmond. Kama kuna mtu ambaye ana ushahidi kuhusu mimi kuhusika apeleke mahakamani vinginevyo akae kimya,” alisema na kusababisha shangwe ukumbini.

Alisema mikono yake ni misafi katika suala hilo na anashangaa wanaomchukia wamethubutu hata kupuuza maelezo yanayotolewa kuhusu suala hilo lilivyotendeka, ikiwemo yeye kuwahi kusema mara kadhaa kuwa alitekeleza alichoelekezwa na mamlaka ya nchi.

Alisema alipata taarifa za udhaifu wa kampuni hiyo ya Richmond na kuitisha kikao cha majadiliano na wizara pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi ambapo alimtaka kiongozi huyo kumjulisha rais na kupata ushauri wa mamlaka ya juu ya serikalia.

Amesema mamlaka ya juu ndiyo iliyoagiza kuwa zabuni itolewe kwa Richmond. “Nimesema nilijiuzulu ili kuilinda serikali sasa nalaumiwa mimi badala ya kupewa nishani… nimechoka na nasema mwenye ushahidi aupeleke mahakamani,” alisemaa.

Mbali na kujiunga na Ukawa, Lowassa amewataka wanachama wa CCM ambao hawakubaliani na siasa chafu za CCM kujiunga na vyama vinavyounda umoja huo huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya kuandikishwa katika daftari hilo.

Akizungumzia tamko la kukaribishwa na Ukawa lililotolewa jana na wenyeviti wa vyama vinavyounda umoja huo, Lowassa alisema “Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa.”

Viongozi wa Ukawa walitoa salamu zao katika hafla hiyo kufuatia uamuzi wa Lowassa kuhama CCM na kuhamia Chadema. Freeman Mbowe (Chadema) alisema “Tuna imani kubwa sana na Lowassa. Hatupambani na mtu. Tunbapambana na mfumo. Nguvu kubwa atakayokuja nayo itakuwa neema kwa Watanzania.”

Mbowe alisema anamshukuru Rais Kikwete ambaye alisema kuongoza kwake vikao vilivyomkata Lowassa katika kugombea, kumesaidia kumtoa CCM na kuhamia UKAWA.

“Ujio wa Lowassa umezua hofu ndani ya CCM. Kumleta Lowassa Chadema haikuwa kazi rahisi. Nasema ukweli simezi matapishi. Hatuwezi kufikiria mambo mema kwa kufikiria mambo mabaya ya zamani. Hata kama tukichukua dola hatuwezi kuongoza kwa kufanyiana visasi,” amesema Mbowe.

Profesa Ibrahim Lipumba (CUF): Tumeongeza nguvu katika Ukawa kupambana na CCM. Wamesahau hata yale malengo ya kupigania uhuru. Tunamkaribisha.

James Mbatia (NCCR-Mageuzi): Siku ya leo nina amani ya dhati kutoka ndani ya moyo wangu. Wabaya wetu walisema Ukawa tutasambaratika. Watanzania wameshuhudia tukiimarika. Hatua iliyofikiwa na Lowassa ni ya kihistoria. Tutaendelea kulinda haki zako za uwaziri mkuu.

Dk. Emmanuel Makaidi (NLD): Tumpongeze Mbowe kutuletea hiki kifaa kinaitwa Lowassa. Tutakuwa pamoja na kuhakikisha CCM inaondoka madarakani. Sisi tunataka baada ya kuingia Ukawa aache huko mambo ya CCM, afuate ya Ukawa. Tunamtakia maisha mema ndani ya Ukawa.

error: Content is protected !!