July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa: Tutachukua nchi asubuhi

Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa akihutubia Mkutano Mkuu wa chama hicho mara baada ya kumpitisha

Spread the love

EDWARD Lowassa ambaye ni mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema chama hicho kwa ushirikiano na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) watashika dola Oktoba 25 mwaka huu saa 2:30 asubuhi. Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea).

Akizungumza na wajumbe wa chama hicho kwenye Mkutano Mkuu leo jijini Dar es Salaam Lowassa amesema, hakuna sababu ya kutoa lugha za matusi huku akiwasihi kuimarishwa kwa amani wakati wa uchaguzi huo.

“Muungano huu una nguvu kubwa ya kwenda kuchukua dola saa 2:30 asubuhi, na tutachukua dola asubuhi,” amesema Lowassa na kuongeza; “hatuko tayari kuibiwa kura na hatutafanya fujo lakini wasiibe kura zetu.”

Amesema kuwa, katika maisha yake hana msamiati wa kushindwa isipokuwa ana msamiati wa kushinda huku akiwataka wana Chadema na UKAWA kuwa wamoja katika kukidondosha Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

Lowassa amesema, wakati akiwa CCM safari yake ya kwenda Ikulu ilikuwa ‘Safari ya Matumaini’ na sasa ndani ya Chadema kwa usaidizi wa UKAWA safari hiyo inaitwa ‘Safari ya Mabadiliko nje ya CCM.’

Akiwa mwenye kujiamini amesema, changamoto kubwa ipo katika UKAWA kutokana na walio nje ya umoja huo kwa maana ya CCM kufikiria kuuvuruga.

Hata hivyo ameabainisha kuwa, hatua ya Chadema na UKAWA kumwamini na kumkabidhi bendera ya kupeperusha kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni nzito.

“Kazi miliyonipa ni nzito, nasisitiza kuwa sitawaangusha, nitawajibika kwa vitendo,” amesema Lowassa huku akiwahakikishia wajumbe hao kuwa chama hicho na UKAWA watashika dola.

Lowasa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli amesema, hakukurupuka kufikia uamuzi wa kuhamia Chadema na kwamba, alifanya mashauriano na mkewe pamoja watu wanaomzunguka.

Amesema, “sikujiunga Chadema kwa bahati mbaya, nilikaa na mke wangu, familia yangu pamoja na watu wanaonizunguka na kufikia uamuzi huu. Nasema kuwa, kazi ya chama ni kushika dola na tumejiandaa kushika dola. Nitapita kila jimbo la nchi hii kuhakikisha tunachukua majimbo yote, kajiandaeni huko, nakuja.”

error: Content is protected !!