May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa, Sumaye kung’oa ‘kitanzi’ cha JPM?

Mawaziri Wakuu wa Wastaafu, Edward Lowassa (kulia) na Frederick Sumaye ambao wote wamehamia upinzani

Spread the love

DODOMA ni moto. Ni kutokana na Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari wa 2016 utakaojadiliwa kabla ya kupitishwa na kuwa sheria kamili, anaandika Faki Sosi.

Serikali ya Rais John Magufuli imeandaa muswada ambao katika macho ya waandishi wa habari, baadhi ya wanasheria, wanasiasa na wachambuzi mbalimbali wanauona kuwa ni kitanzi cha serikali dhidi ya uhuru wa habari na waandishi nchini.

Edward Lowassa na Frederick Sumaye ambao ni mawaziri wakuu wastaafu, tayari wametua katika ardhi ya Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kukutana na wabunge wa upinzani ili kuongeza nguvu dhidi ya muswada huo ikiwa ni pamoja na mambo mengine.

Taarifa za kuwepo kwao Dodoma zinachagizwa na msimamo unaooneshwa na serikali dhidi ya muswada huo, lakini je, watasaidia kushawishi kuurudisha njuma?

Lowassa ambaye pia alikuwa mgombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Sumaye watakutana na wabunge wa upinzani ili kuweka mikakati dhidi ya hoja mbalimbali za serikali zitakazoonekana kutokuwa na maslahi kwa Watanzania.

“Ni kweli wamekuja hapa kwa malengo ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Watakutana na wabunge wa upinzani ili kuhakikishwa wanakuwa na kauli moja katika masuala ya kitaifa,” amesema John Marema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema.

Vikao cha Bunge mjini Dodoma vinatarajia kuanza kesho ambapo tayari baadhi ya wabunge wamewasili mjini humo kwa ajili ya maandalizi ya vikao hivyo.

Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari wa Mwaka 2016 ni miongoni mwa miswada itakayojadiliwa na tayari Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ameuwasilisha kwa Kamati ya Huduma za Jamii.

Ukawa ni miongoni mwa wadau wa habari ambao wamejitokeza na kuonesha upungufu mkubwa uliomo kwenye muswada huo.

Wamekuwa wakieleza kwamba, endapo utapita, utafunga vyombo vya habari, waandishi pamoja na kufinyanga uhuru wa habari.

Muswada huo pia umeendelea kulalamikiwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambalo limeeleza kwamba, una upungufu mkubwa na unahitajika kufanyiwa uchambuzi zaidi.

Pia TEF imeliomba Bunge kutoharakisha kuuwasilisha na badala yake uwasilishwe katika Bunge la Februari mwakani baada ya kufanyika kwa marekebisho hayo.

Kali hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Theophil Makunga, Mwenyekiti wa TEF na kwamba, muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Septemba mwaka huu lakini bado kuna kasoro kadhaa katika baadhi ya vifungu kuanzia cha 12 hadi 55.

Akianisha vipengele vinavyoonekana kandamizi kwenye muswada huo Deodatus Balile, Makamu Mwenyekiti wa TEF amesema, ni pamoja na kifungu cha 12 ambacho kimeipa mamlaka bodi kufanya ithibati na kutoa Press Card, wakati kazi hiyo inaweza kutolewa na Baraza Huru la Habari.

“Kifungu cha 13(a) kinasema mwandishi akishaondolewa katika orodha ya wanahabari haruhusiwi kufanya kazi kwenye chombo chochote cha habari au taaluma inayohusiana na mambo hayo, jambo linaloonyesha wazi kuwa uamuzi huo ni wa kummaliza mwanahabari hata kama alifanya kosa kwa bahati mbaya,” alisema Balile.

Kingine ni kifungu cha 47 ambacho kinasema mwanahabari atakayekutwa na kosa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano hadi 20 au kifungo cha miaka mitatu jela au kisichopungua miaka mitano.

“Na kifungu cha 50 kinasema mtu yeyote yule hata kama siyo mwanahabari atakayekutwa na chapisho la uasi anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni mbili au isiyozidi Sh milioni tano na ikiwa amerudia kosa hilo atafungwa miaka mitatu jela.

“Mbali hilo na pia kifungu cha 55 katika muswada huo kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana kufuta chombo chochote cha habari huku Kifungu cha 60 (a) Waziri anatakiwa kutunga kanuni ya utoaji wa taarifa ya vyanzo vya mapato kwa vyombo vya habari wakati vyombo hivyo baadhi yao vinamilikiwa na watu binafsi,” amesema Balile.

error: Content is protected !!