July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa: Ole wenu NEC

Spread the love

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ameionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi kuchochea vurugu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Onyo la Lowassa limekuja ikiwa imebaki siku moja kabla ya Watanzania kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa rais, ubunge na madiwani.

Akihutubia wakazi wa Ifakara Jimbo la Kilombero, Morogoro leo mchana katika Uwanja wa Shule ya Jagwani, Lowassa amesema “polisi waache kuwafuatafuata vijana wetu na kuwapiga.”

Lowassa amesema, “Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanapaswa kutambua kwamba, uchaguzi huu ni muhimu. Watu wamejitolea kujiandikisha na kwenda kupiga kura ifika Jumapili, watu hawa wana matumaini. Tume itende haki.”

Mbali na onyo hilo, Lowassa amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, ataanza kutatua changamoto za sekta ya elimu kwa kutoa elimu bure kwanzia Shule ya Msingi hadi Chuo Kikuu.

“Mbali na elimu, kipaumbele changu cha pili ni kilimo. Nitahakikisha tunakuwa na kilimo cha kisasa cha umwagiliaji. Mkulima atakuwa na haki zake. Serikali yangu itafuta ushuru wa mazao yote. Wakulima watauza mazao popote watakapotaka duniani,” amesema Lowassa.

Kuhusu maslahi ya wafanyabiashara ndogondogo na wenyeviti wa vijiji amesema “mimi ni rafiki wa bodaboda, mama lishe na machinga. Nikiingia madarakani nitaanzisha benki maalum kwa ajili ya makundi haya. Pia nitawalipa mishahara wenyeviti wa vijiji,” amesema Lowassa.

Lowassa ameahidi kutatua kero za Jimbo la Kilombero ambalo linawakilishwa na mgombea Peter Lijualikali kwa tiketi ya Chadema.

“Kero zinazowakabili wananchi katika jimbo hili ni kutozwa ushuru kwa wakulima wa mpunga, tatizo la maji, watu wa Sanje kudhulumiwa ardhi yao, kutokamilika kwa daraja linalounganisha Mahenge, Kilombero na Malindi na kivuko kilichopo muda wowote kinaweza kuzama,” amesema Lijualikali.

Aidha, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amewataka wananchi kuwahi katika vituo vya kupigia kura huku kila mpiga kura kubeba kalamu yake badala ya kutegemea kalamu za maofisa wa NEC.

“Tuwahi katika vituo vya kupiga kura alfajir. Kazi ya kwanza Jumapili ni kupiga kura, kila mtu aende na kalamu yake. Mtu ambaye hajui kusoma na kuandika amchukue mwenzake anayemwamini,” amesema Sumaye.

Mbali na wito huo, Sumaye amewataka mawakala wa watakaolinda kura za vyama vinavyounda Ukawa kutohadaika na rushwa itakayotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kuna dalili kwamba CCM wanataka kuwanunua mawakala wetu. Kweli unakubali kupewa Sh. 20,000, 30,000 au 50,000 halafu mtoto wako atesekeke miaka mitano kwa kukosa dawa? Wakala wetu siku hiyo unapokwenda kwenye kituo chako cha kazi, uwe umekula nyumbani. Usiende kudoea chai inayoletwa humo, huwezi kufa kwa njaa kwa siku moja,” amesema Sumaye.

error: Content is protected !!