January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa: Nitakuwa mfano kwa Kikwete

Spread the love

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amesema, akiingia Ikulu atakuwa mfano kwa marais waliomtangulia. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Miongoni mwa marais watakaokuwa kwenye orodha ya kumtangulia Lowassa iwapo ataingia Ikulu ni Rais Jakaya Kikwe ambaye ameanza kuongoza taifa hili mwaka 2005 mpaka sasa.

Lowassa ni mgombea urais wa Chadema pia mwakilishi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ni Chadema yenyewe, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Lowassa amesema, katika kipindi cha miaka 10 ya Rais Kikwete aliyokaa madarakani ameliingiza Taifa kwenye umaskini na ameshindwa kutekeleza ahadi zake.

Amesema, kutokana na CCM kushindwa kusimamia na kutekeleza ahadi zake, akiingia Ikulu atahakikisha nchi inapata maendeleo.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akihutubia maelfu ya Watanzania katika uwanja huo na kwamba, baadaya ya Oktoba 25 kuingia Ikulu atakuwa mfano kwa marais hao waliomtangulia kwamba namna gani nchi inaongozwa na kukuwa kiuchumi.

Amesema muda wa kampeni haujafika, lakini kutokana na kufahamu changamoto na ahadi hewa zilizotolewa na Rais Kikwete, atazitatua katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

Lowassa amesema Rais Kikwete alahidi ahadi nyingi wakati wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali ikiwamo Mwanza ambao waliahidiwa Treni ya mizigo na abiria, kujengewa soko kubwa la Machinga Complex, kufufua viwanda na tatizo la umeme lililipo mpaka sasa kwa hivyo vyote atavishughulikia.

Amesema, Watanzania wanakabiliwa na janga kubwa la umaskini na kwamba, anamuomba Mungu kupata urais ili kubadilisha maisha yao.

Oktoba 25 mwaka huu anasema, akiingia Ikulu ataunda serikali inayochapa kazi na kuendesha nchi mchakamchaka wa hali ya juu na kwamba, kwa mtumishi mzembe hata vumiliwa ataondolewa.

Amesema, licha ya Tanzania kuwa na raslimali nyingi lakini bado nchi hiyo imezidiwa na nchi ambazo hazina vitega uchumi, kama Rwanda, Kenya na hata Burundi.

CCM kupelekwa ICC

Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu amesema, watumishi wa Jeshi la Polisi na viongozi wa CCM watakaosababisha nchi kuingia katika machafuko katika Uchaguzi Mkuu watawashitaki Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

“Jana (Juzi) Arusha Polisi walipiga msafara mabomu lakini leo nimesikia kwamba wamepiga inasikitisha sana.

“Wanawatuma na polisi wao wajiandae kwenda kujibu mashitaka ICC… tutawapeleka wachukuwe mfano wa Kenya ambao wapo huko wanaozea huko hawajarudi na nyie mtaozea huko,” amesema.

Mbowe na JWTZ

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Davis Mwamunyange kwamba waache kuingilia masuala ya uchaguzi na kuendelea kulinda amani iliopo.

Amesema, Chadema na Ukawa kwa pamoja wanamtaka Mwamunyange asilitumie jeshi hilo vibaya kuisaidia CCM kwani mishahara wanayolipwa polisi ni kodi za Watanzania wote.

“Kuna vijana watatu ambao wanasifika kwa utalamu wa computa wameenda Tume ya Taifa Uchaguzi kufanya kazi na wapo pale hawajitambulishi kama wanajeshi na mchezo wanaoufanya tumeufahamu na waache mara moja na kwamba kama ni ushahidi anao na hakuna kitu watakachokifanya wasikifahamu,” amesema.

Hali ilivyokuwa

Lowassa alipowasili uwanjani hapo na kupanda jukwani alishangiliwa na maelfu ya wananchi hao huku wakimuita rais, rais, rais, … na kumfanya mgombea huyo kupata kiwewe kutokana na shangwe za wananchi na wafuasi wa UKAWA.

Lowassa amesema, kujaa kwa wananchi hao kumeonesha dhahiri ni nguvu ya umma ndani ya UKAWA na kuwaahidi kutowaangusha akiingia Ikulu katika kuwapelekea maendeleo.

Msafara wa Lowassa ambao ulitua Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 6:30 mchana ukitokea Arusha alikofanya mkutano juzi na kuhudhulia na watu wengi ambao hata hivyo hawakufikia wa jana Mwanza.

Katika msafara huo ambao aliongozana na mgombea mwenza, Juma Haji Duni na safari ya kuelekea uwanja wa furahisha ilianza saa 8:00 mchana na kufika saa 9:40 alasiri ambako huko watu walikutwa wamefurika huku watu zaidi ya 10 wakizimia kutokana na uwanja kujaa.

Msafara huo ambao ulikuwa wa aina yake ambako watu walioandama waonekana wakifagia barabara ili gari lililimbeba Lowassa lipite eneo safi, wengine wakiwa na mfano wa jeneza linaloashiria kufa kwa CCM.

Nyomi ya watu barabara walisimama kumlaki na wingi wao unazidi wa ule alikokwenda kuchukua fomu ya Serikali ya kugombea Urais NEC jijini Dar es salaam.

Hata hivyo, katika msafara huo ambao uliongozwa na vijana awali walitimuliwa kwa mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi.

Mabango

Baadhi ya mabango yaliokuwa yamebebwa na wananchi hao yalisomeka tofauti ikiwemo ‘Lowassa Lowassa ulipo tupo twenzetu Ikulu’, ‘Ni Bora Ebola kuliko kuongozwa na CCM’, ‘Funguo za Magufuli ni Lowassa na ‘Chadema usipime utaunguzwa’.

error: Content is protected !!