July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama Kuu: Lowassa msafi

Spread the love

MGOMBEA Urais wa Tanzania, Edward Lowassa anayewakilisha UKAWA – Umoja wa Katiba ya Wananchi – kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo amewasilisha Hati ya Kiapo mbele ya Mahakama Kuu ikiwa ni hatua ya ukamilishaji utaratibu kwa mgombea nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Lowassa ambaye Agosti 10 alitinga makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za uteuzi wa kuwania nafasi hiyo, katika safari ya kukutana na Jaji, alifuatana na Mgombea Mwenza wake, Juma Duni Haji, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, wakili Mabere Marando.

Ujumbe wa mgombea ulifika mbele ya Jaji Suleiman Said Komu, ambaye alifanya kazi ya kuzipitia fomu hizo kwa hatua muhimu ya kuzihakiki kabla ya kuziwasilisha NEC kwa hatua ya kusubiri kuteuliwa kama hakutakuwa na pingamizi yoyote.

Mwanasheria na wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar, akizungumza kwa sharti la kutotajwa kwa jina, ameiambia MwanaHALISI Online kwamba hatua ya kusaini Hati ya Kiapo ni muhimu kwani inathibitisha kuwa fomu za uteuzi zimejazwa vizuri na hakuna tatizo.

“Ni hatua ya lazima kwa kila mgombea urais kwenda kuhakikiwa fomu zake kabla ya kuzirudisha tume ya uchaguzi. Utaratibu kama huu upo pia kwa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo inataka mgombea urais awasilishe fomu zake Mahakama Kuu kwa ajili ya kuthibitishwa,” alisema wakili huyo.

Lowassa ambaye kwa hatua hiyo maana yake amethibitishwa kuwa ni mgombea asiye kasoro ya kisheria, anatarajiwa kurudisha fomu hizo NEC saa 4 asubuhi siku ya Ijumaa.

Hatua kama hiyo aliitekeleza mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli akifuatana na mgombea mwenza wake Samia Suluhu Hassan, anayetokea jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Unguja. Walifika mbele ya Jaji Sekiete Kihiyo.

Kwa kila aliyechukua fomu za uteuzi NEC, atapaswa kuzirudisha muda wa mwisho ukiwa ni Agosti 22, siku ambayo Tume ya Uchaguzi imetangaza kuwa ndio mwanzo wa safari ngumu ya kampeni itakayodumu kwa miezi miwili hadi Oktoba 25, siku ya upigaji kura kuchagua Rais, wabunge na madiwani.

error: Content is protected !!