August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa, Lissu ‘kutia timu’ BAVICHA

Spread the love

EDWARD Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anatarajia kuhudhuria kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) Mkoa wa Dodoma, anaandika Dany Tibason.

Tundu Lissu, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni pia Mbunge wa Iramba Mashariki ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kwenye kongamano hilo ambalo Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema ndio mgeni rasmi.

Kwenye uzinduzi wa kongamano hilo, kutakuwepo na mada tatu ambazo ni nafasi ya vijana katika siasa na hali ya ajira katika taifa ambayo mchokoza wa mada hiyo ni John Heche, Mwenyekiti Mstaafu (BAVICHA) pia Mbunge wa Tarime Vijini.

Mada ya pili itakuwa utawala wa sheria katika Serikali ya Awamu ya Tano ambapo Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini atakuwa mchokonozi.

Mada ya tatu itakuwa wa watumishi wa umma na wanavyuo katika siasa na haki ya kupiga kura ambapo mchokoza mada hiyo ni Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari Manyanya Marambaya Manyanya, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana   Mkoa wa Dodoma amesema, vijana hao kwa kushirikiana na Umoja wa Wananchadema Vyuo Vikuu (CHASO) wameandaa kongamao hilo kwa lengo la kutoa elimu kwa vijana na jamii juu ya mustakabali wa taifa.

Manyanya ameeleza kuwa, kwa sasa katika uongozi wa awamu ya tano kuna sheria nyingi na haki za binadamu zinavunjwa kutokana na utawala uliopo madarakani jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mbali na hilo amesema, kutakuwepo na mada mbalimbali ambazo zitakuwa zikitoa mwelekeo wa uongozi wa awamu ya tano ambao unaonekana kuvunja haki za watumishi pamoja na kuminya uhuru wa kisiasa kwa watumishi ambao wanataka kufanya siasa.

“Kwa sasa hatuwezi kupata mabadiliko ya kweli kutokana na serikali iliyopo madarakani ambayo inatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Ni aibu kwa watu ambao walituhumiwa kuhusika katika ufisadi na kashifa ya uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ambao kwa sasa wamerudi katika baraza la Mawaziri katika utawala wa awamu ya tano” amesema Manyanya na kuongeza;

“Tuliona utumbuaji wa majipu kwa Daktari wa Mtwara baada ya Waziri Mkuu kumtumbua jibu Dk. Wagonjwa nao kwa sasa wanaonekana kujichukulia hatua za kuwapiga wauguzi jambo ambalo linaonekana kuwa baya na halistahili kwa jamii.

“Lakini tumekuwa tukishihudia jinsi watumishi wanaponyimwa haki zao za kujitetea na bila uchunguzi wa kutosha kama anayetumbuliwa jipu ndiye muhusika mkuu wa tatizo au la, hivyo kongamano hili litaweza kutoa elimu kwa vijana na jamii ambao watakuwa katika kongamano hilo sambamba na kutambua haki zao za kisiasa na haki za kawaida ambazo ni haki yao kuzipata.”

Manyana amesema kongamano hilo litahudhuriwa na wabunge wa Chadema wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Dodoma pamoja na umoja wa wanachadema kutoka Sekondari (CHASESO) pamoja na nafasi 200 kwa wananchi wa kawaida kutoka vyama mbalimbali vya siasa.

error: Content is protected !!