July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa karibu Kilwa J’tano

Spread the love

WAKAZI wa wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi, Jumatano watashuhudia ugeni mzito wa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema, anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa, atakapowasili kwa ajili ya kampeni ya kuomba kura. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Lowassa ameshaanza kupita majimboni kwa kutumia helikopta, atafanya mkutano mkubwa saa 8 mchana kwenye uwanja wa mpira wa Msagamoni, Kata ya Kipatimu.

Kwenye mikutano yake, Lowassa ambaye alihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) katikati ya mwezi uliopita, baada ya kukumbana na mizengwe katika uteuzi wa wagombea, anafuatana na timu kabambe ikiongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.

Sumaye naye alijiunga na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) baada ya CCM kuteua mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli, akiwa mmoja wa wanachama 34 waliorudisha fomu za kuomba uteuzi wa chama hicho.

Sumaye pia aliomba ridhaa ya kuteuliwa lakini alipohama chama alisema sababu ni kutoridhika na utaratibu wa uteuzi ulivyofanyika na pia kuamua kujiunga na Lowassa ili kusaidia kampeni ya mabadiliko wanayoyataka wananchi walio wengi.

Hata hivyo, wakati Lowassa haraka alitambulishwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maende,leo (CHADEMA), Sumaye aliyetumikia uwaziri mkuu kwa miaka kumi mfululizo chini ya rais Benjamin Mkapa (Npvemba 1995/Oktoba 2005), hajajiunga na chama mahsusi kati ya vile vinne vinavyounda Ukawa.

Chadema katika umoja huo wanashirikiana na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD). Mgombea mwenza wa Lowassa ni Juma Dunia Haji ambaye jana alirejea mkoani Tabora kukamilisha safari ya kampeni mkoa ambao Lowassa alitangulia kupita mapema mwezi huu.

Katika mikutano yake kwenye mikoa 15 kufikia leo, Lowassa anafuatana na Sumaye pamoja na Khamis Mgeja aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mwanasheria wa Chadema na mgombea ubunge Singida Mashariki, Tundu Lissu na Meneja wa kampeni yake Lowassa, John Mrema.

Lowassa jioni hii anakamilisha safari ya kampeni jijini Dar es Salaam katika majimbo ya Kigamboni, Mbagala na Ukonga. Tayari ameshapita Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Geita, Simiyu na Kagera.

Anaingia mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara ambako Duni, mwanasiasa mahiri aliyelazimika kuhama CUF ili kupata kuwa mgombea mwenza kulingana na maafikiano ya UKAWA, alianzia safari ya kampeni.

error: Content is protected !!