January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa hajavunja utaratibu – Mbatia

Spread the love

MWENYEKITI Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), James Mbatia amesema mgombea urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amelazimika kuzungumzia suala linalohusu watuhumiwa walioko mahakamani kutokana na vilio vya wananchi alikopita. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mbatia amesema Lowassa ambaye anagombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amekuwa akiulizwa nini atafanya kuhusu masheikh waliofunguliwa mashitaka ya tuhuma za ugaidi pamoja na wanamuziki ndugu wanaotumikia vifungo gerezani kwa kosa la kubaka na kulawiti.

Kuna masheikh wapatao 20 kutoka Zanzibar walikamatwa mwaka 2013 na kuhamishiwa Dar es Salaam ambako wamefunguliwa mashitaka lakini kwa miaka miwili sasa kesi zao zinaendelea kupigwa danadana huku wakilalamika kuwa wamedhalilishwa na kuteswa na wanaamini wamefunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya kutoa maoni yao kuhusu katiba na muungano.

Aidha, mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na mwanaye Johnson Nguza (Papii Kocha) wamekuwa wakitumikia vifungo gerezani lakini kumekuwa na malalamiko kuwa tuhuma dhidi yao zilitengenezwa kwa sababu ya chuki.

Mbatia amesema kwa sababu Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji wamekuwa wakiulizwa kwingi waendako na kukutana na wananchi, wanawajibika kutoa maelezo ya kuangalia utaratibu wa kisheria na utawala bora kuona cha kufanya.

“Ni fikra potofu kuhusisha suala la ugaidi na imani ya dini. Lowassa alisema atafuata misingi ya kikatiba, kisheria kuangalia ukiukwaji wa taratibu katika hukumu zilizotolewa ili sheria ifuate mkondo wake,” amesema Mbatia.

“Katiba yetu ya sasa, Ibara ya 9(a) inasema utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa; (f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni la Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu,” amesema mbele ya waandishi wa habari.

Amesema kauli ya Lowassa imekuwa ikipotoshwa kwamba akichaguliwa kuwa rais atatumia nguvu kuwatoa masheikh na viongozi wao kutoka Jumuiya ya Uamusho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) pamoja na Babu Seya na mwanaye.

Amesema suala hilo lilijitokeza katika mikutano ya Ukawa iliyofanyika Mbeya, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na Zanzibar ambako wananchi walilalamikia walichoita “ukiukwaji wa sheria” na kutolewa hukumu zisizozingatia haki ndio maana “amelazimika kuzungumzia hayo na hajakiuka utaratibu kwani amesema atatumia utawala wa sheria kuona kama haki imetendeka.”

Mnamo 25 Juni 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Addy Lyamuya alitoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kubaka na kulawiti watoto wa Shule ya Msingi, Sinza Mashujaa, jijini Dar es Salaam.

Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao.

Kupitia kwa wakili wao maarufu nchini, Mabere Marando, wawili hao waliwasilisha rufaa ya pili ambayo pia ilikataliwa. Mwaka 2010, waliomba marejeo ya uamuzi wa rufaa yao hiyo na uamuzi ukawa kuwaondolea adhabu Nguza Mbangu na Francis Nguza huku ikiendeleza adhabu kwa Babu Seya na Papii.

Masheikh na viongozi wa Uamsho walifikishwa mahakama ya Kisutu mwaka 2013 lakini mpaka sasa kesi hazijasikilizwa huku wakiwa wameendelea kukaa gerezani kwa vile haki yao ya dhamana imefungwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Tanzania.

Mei 23, mwaka huu viongozi hao walimwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kumweleza wanavyopata mateso kama vile kuhojiwa wakiwa uchi wa mnyama, kulawitiwa na kuwekewa vijiti sehemu za siri, kupigwa hadi kuzimia na kutoka taya, kulazwa na pingu huku wakining’inizwa hadi asubuhi.

Wanadai mateso hayo yamewafanya kuendelea kupata maumivu, kutokwa na haja kubwa ovyo, kupoteza fahamu na kukojoa damu.

Barua yao inasomeka: “Waziri Mkuu dai letu ni moja tu kusema kwamba bado serikali ya CCM inamdanganya Rais Jakaya Kikwete, basi sisi Wanzanzibari dai letu turejeshwe nchini kwetu Zanzibar.”

“Kwa kuwa kesi hiyo ni ya kubuni kwa malengo machafu ya kisiasa ndio sababu ya kushtakiwa katika mahakama ya Kisutu. Tumebambikiwa kesi ya ugaidi kutokana na msimamo wetu wa wazi wa kudai mamlaka kamili ya nchi ya Zanzibar,” wanasema.

Wanasema msimamo huo waliutangaza nchi nzima kupitia mikutano ya hadhara chini ya taasisi za Kiislamu za Zanzibar na kuendeshwa na JUMIKI kwa kufuata taratibu zote na sheria za nchi.

“Kilichofuata ni serikali ya CCM kuwashughulikia wale wote wanaonadi au vinara wa msimamo huo, ushahidi wa hayo ni kuwa hawakusalimika hata kidogo ndani ya chama,” inasomeka.

“Baada ya malalamiko hayo, tumefanya uchunguzi na kubaini katika mifumo yetu ya kisheria na magereza kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hata Tume ya Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wametoa ripoti kulaumu jambo hili…. moja ya kipaumbele chetu ni kulinda utu na haki za Watanzania,” amesema Mbatia.

error: Content is protected !!