July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

99.3% zawavusha Lowassa, Duni Urais 2015

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa (kushoto) akifuatiwa na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji. Kulia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad

Spread the love

WANACHAMA wapya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Juma Duni Haji wamepitishwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kugombea ngazi ya urais na umakamu wa rais kwa asilimia 99.3. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Jumla ya wajumbe 2,021 kati ya 2,035 waliotakiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo, waliwapitisha wajumbe hao wapya kwa kishindo katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam leo.

Lowassa aliyeteuliwa kugombea urais, alijiunga na chama hicho Julai 28 mwaka huu. Duni maarufu kama Babu Duni ambaye ndio mgombea mwenza wake akijiunga na chama hicho jana.

Duni alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), pia Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambapo nafasi hizo mbili alizivua jana na kisha kujiunga Chadema.

Babu Duni alilazimika kuvua nyadhifa hizo ili kutii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayelekeza chama kinachosimamisha rais ndio kitachosimamisha mgombea mwenza.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa makubaliano ya pamoja ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kukubaliana kuunda nguvu ya pamoja ili kukikabili Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Katika mkutano huo, utaratibu uliotumika kupitisha wagombea hao ni kura ya wazi ambapo kanda 10 za chama hicho kila moja iliposimamishwa ilipiga kura ya ‘ndio’.

Mratibu wa shughuli ya upigaji kura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe alitaja kuwepo kwa kanda 10 zilizoundwa na chama hicho ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kati, Magharibi, Kusini, Pwani, Pemba, Unguja, Nyasa, Serengeti na Nyanda za Juu Kusini.

Hata hivyo, wakati wa kumpitisha mgombea mwenza (Duni), ni mjumbe mmoja kutoka Kanda ya Pemba aliyesimama na kupinga uteuzi wake.

Akizungumzia utaratibu wa kuteua mgombea huyo Mbowe amesema kuwa, kwa mujibu wa katiba hiyo kifungu namba 7.16, mgombea urais pamoja na makamu wake wanateuliwa na sio kupigiwa kura.

Mbele ya wajumbe hao pamoja na wageni waalikwa kutoka nchi na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi Mbowe amesema, “Jana Baraza Kuu lilikubali kwa asilimia 100 mapendekezo ya Kamati Kuu ya kumteua Duni na Lowassa kuwa wagombea wetu.”

Hata hivyo, Mbowe amesisitiza kuwa, katika kumkaribisha Lowassa kwenye chama hicho, Dk. Willibrod Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho alihusika na aliridhia.

“Narudia Kamati Kuu yote iliridhika kumkaribisha Lowassa akiwemo Dk. Slaa,” na kuongeza “lakini pengine nguvu za pembeni zikashauri tofauti.”

Kauli kuwa ‘nguvu za pembeni zilishauri vingine’ ililenga kuwepo kwa sintofahamu kati ya chama hicho kuhusu ujio wa Lowassa na msimamo wa Dk. Slaa unaoonekana kupinga hatua hiyo.

Mbowe amewaambia wajumbe hao kuwa, nchi hii ina ndoto ya mabadiloko na kwamba, mpaka sasa kazi kubwa imefanywa na Chadema pia vyama washirika wa UKAWA na hata leo kuwa wamoja.

“Vimefanyika vikao vingi ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto hii ya kitaifa, umoja wetu hautenganishwi kwa misingi ya ukabila, rangi, dini. Tunamuhitaji kila mtu mwenye malengo chanya kuungana nasi,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Hatuwezi kujenga uadui wa kudumu, tunahitaji karama ya kila mtu kuunda jeshi la umoja ili kufikia ndoto yetu. Ndoto ya taifa letu ni kubwa kuliko matumaini ya kila mmoja wetu.”

Amefafanua kuwa, chama hicho kinatambua kwamba wapo kwenye umoja katika safari hiyo na kwamba, kila chama kina uwezo wa kusimamisha mgombea wake ngazi zote lakini kutokana na kuwa na doto ya aina moja, wamekubali kuungana ili kuitimiza.

Amekumbusha kuwa, katika kuelekea kukamilisha ndoto hiyo, vyama hivyo vimepigana kwa zaidi ya miaka 20 na kuwa, wapo waliopoteza maisha, waliopata ulemavu na wengine kuachika katika harakati hizo.

Hata hivyo, aliwakaribisha wanachama wengine waliopo nje na kuongeza kuwa “Chadema nchi nzima hatuna haki ya kuwahukumu wanaohamia.tuwatie moyo na kuwakaribisha vizuri ili ndoto itimie.

“Sisi wote ni wanaadamu, tuna mapungufu. Wapo watu watatoka nje na kuja kuishi na sisi kama wana Chadema. Sisi ni chama cha siasa, chama cha siasa ni watu na sio mahakama. Namkaribisha Lowassa.”

Mbowe mesema “Mabaya ya chama cha zamani tumeyasamehe, tunayaomba mazuri yote mliyoyapata huko mtuletee.”

Pia Mbowe alieleza wasifu wa wagombea wa chama chake na kuwataka wajumbe, wanachama na wananchi kutokuwa na mashaka na wateule hao.

error: Content is protected !!