July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa atua Arusha, Mgeja alaani polisi Kagera

Spread the love

EDWARD Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika uchaguzi mkuu mwaka jana ameingia jijini Arusha leo akitokea mkoani Kagera ambapo alizuiliwa kufanya mikutano ya ndani na Jeshi la Polisi la polisi, anaandika Charles William.

Ni jana tu Jeshi la Polisi kupitia Nsato Marijani, Kamishina wa Operesheni na Mafunzo lilitangaza kuruhusu mikutano ya ndani ya vyama vya siasa pamoja na ile ya hadhara ya wabunge, hata hivyo hali imekuwa tofauti mkoani Kagera, Ijumaa ya leo.

Akiwa ameambatana na Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini pamoja na Khamis Mgeja, mwanachama wa Chadema, Lowassa aliwasili Kagera leo asubuhi kwa lengo la kutoa msaada kwa wahanga wa tetemeko la ardhi.

“Tulipokuwa tukitembelea wahanga, polisi walikuwa wakitufuata nyuma kila tulipoenda, wakiwa na magari yao yenye askari waliokuwa na silaha za moto ikiwemo mabomu ya machozi,” ameeleza Mgeja ambaye alikuwa ameambatana na Lowassa katika msafara huo na kuongeza;

“Tumeshangazwa sana na kitendo hiki kwasasbabu Lowassa ni mtu wa amani na anatambulika hivyo duniani kote inakuaje afuatwe na polisi wenye silaha za moto ilihali ameenda kutoa msaada tu na katika msafara wake hakuna mtu hata mwenye manati ya kudhuru watu?” amehoji.

Baada ya Lowassa kumaliza kutembelea wahanga wa tetemeko la ardhi ametoa msaada wa mifuko 400 ya saruji ambayo amemkabidhi Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ili kuwafikishia wahanga hao huku pia akipokea taarifa ya maafa kutoka kwa Mkuu huyo wa Mkoa.

Hata hivyo, Lowassa amezuiliwa na Jeshi la Polisi kufanya mkutano wa ndani uliokuwa ufanyike katika ukumbi wa St. Theresa mjini Bukoba kwasababu ambazo hazikujulikana mara moja.

Akizungumza na MwanaHALISI online kwa njia ya simu, Mgeja amesema, Lowassa kama mwanachama wa Chadema na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, alitaka kuwasalimia wanachama wenzake katika kikao cha ndani, jambo ambalo ni la kawaida na hawajui kwanini polisi wamezuia.

“Tunalaani kitendo hiki na tunamtaka Ernest Mangu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), pamoja na Rais John Magufuli, wawajulishe polisi kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utulivu.

Hakuna sababu ya polisi kujihami kwa mavazi ya kivita na silaha za moto ikiwemo mabomu kisa Lowassa yupo sehemu, huko ni kutumia nguvu kubwa katika mambo madogo. Ni kuwatia hofu wananchi pasipo ulazima,” amesema.

Si mkutano wa ndani wa Lowassa pekee uliozuiliwa, bali hata mkutano wa hadhara wa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Jimbo hilo nao ulizuiliwa na polisi wenyewe licha ya kuupa na kibali hapo awali.

“Mkutano wa Mbunge ulikuwa ufanyike katika viwanja vya Kashai, umeombwa tangu juzi na ulikuwa una kibali, lakini baada ya Lowassa kuingia Bukoba, polisi wameuvunja na kusambaratisha watu kwa mabomu ya machozi,” amesema mtoa taarifa wetu kutoka Bukoba.

error: Content is protected !!