July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa ahofia CCM, agoma kuongea kwenye bonanza

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akiwa katika maandamano ya kupinga mauaji ya Maalbino yaliyofanyika kwenye Viwanja vya TCC Chang'ombe, Temeke

Spread the love

EDWARD Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, amekiogopa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – na kushindwa kueleza hatima ya kinachoitwa, “kushawishiwa kugombea urais, katia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.” Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Hayo yametokea katika bonaza lenye ujumbe, “Tunalaani na Kupinga Mauaji ya albino.”  Bonanza hilo liliandaliwa na Temeke Family Joggig Club. Lilifanyika katika viwanya vya TCC Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Hofu ya Lowassa kuzungumza hatma ya “urais wake” kupitia  bonaza hilo, imetokana na kuonywa na chama hicho, kuacha kutumia makundi mbalimbali ya kijamii kusaka urais.

Mbunge huyo wa Monduli (CCM), ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika bonaza hilo.

Ilikuwa hivi: Alipotakiwa kuzungumza katika hafla hiyo na waandaaji wa bonaza hilo, Lowassa alisema, “Nawashukuru kwa kunialika. Lakini ili nisipate ugomvi na CCM, kwamba nautumia ukumbi huu kwa mambo yangu ya kisiasa, basi namwachia Abbas Mtevu (mbunge wa jimbo la Temeke) yeye atazungumza.”

Akaongeza, “Lakini kwa haya mauaji ya Albino, yanatufanya tuonekane ni majambazi. Yanatuharibia sana sifa. Albino 76 waliouwawa si wachache. Ni maisha ya binadamu.”

Alisema, “ Naiomba serikali kuunda kamati, ili kwa pamoja tuchukue hatua kama nchi.”

Lowassa ameungana na wanachama wa Clabu hiyo kutembea umbali wa kilometa 5 kwa mwendo wa dakika 25 katika maeneo ya barabara ya Taifa, barabara ya Mandela, barabara ya Temeke, barabara ya Chang’ombe na kuishia katika viwanja vya TCC Chang’ombe.

Hatua yake ya kutembea umbali mrefu kiasi hicho, kumeziba madai ya baadhi ya wapinzani wake waliokuwa wakisema afya ya mwanasiasa huyo iko shakani.

Naye Ernest Kimaya, mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ualbino nchini alisema, mauaji ya watu wenye ualbino yaliongezeka kwa kasi nchini kuanzia mwaka 2006.

“Hadi hivi sasa wameuawa watu wenye ualbino 75 na waliojeruhiwa kwa kukatwa viungo ni watu 35. Tunasikitika kukueleza kuwa makaburi 15 yamefukuliwa ili kuchukua viungo vya ndugu zetu waliofariki dunia,” ameeleza Kimaya kwa sauti iliyosheheni majonzi.

Amesema, mauaji hayo ya Albino yanafanya chama chake kuwa na mzigo mkubwa wa kuelimisha jamii na kutatua matatizo yanayowapata huku kukiwa na uhaba wa rasilimali fedha.”

Kimaya amesema changamoto zilizopo ni kwamba watu wenye ualbino wana matatizo ya kupata kansa ya ngozi na uoni hafifu.

“Suluhisho la kumaliza tatizo hili ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii, ili kusaidia kuona Albino ni sehemu ya jamii yao, kuwashirikisha katika masuala ya ujenzi wa taifa letu na vyombo vya usalama kujipanga sawasawa na kukabiliana na wale wanaosababisha madhara haya,” ameeleza.

Salim Ahmed Salim, ambaye ni msemaji msaidizi wa Clab hiyo amesema, dhumuni la bonaza hilo ni kulaani na kupinga mauaji na ukataji wa viungo vya Albino.

Lengo lingine ni kuwaambia umma kuwa Albino ni binadamu kama binadamu wengine. Wanastahili upendo furaha na kuishi bila ya kupata huzuni na hofu katika mioyo yao.

Alisema shirika lake, linakusudua kufika katika mikoa iliyokithiri kwa mauaji ya Albino kama vile Mwanza, Shinyanga na Tabora ili kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki kuwalinda watu wenye ualbino.

Aidha, ziara hiyo itatumika kuitaka serikalia na vyombo vyake vya usalama wa raia kuwa na mkakati madhubuti wa kuwalinda watu wa jamii hiyo.

error: Content is protected !!