June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa ambana Kikwete

Spread the love

EDWARD Lowassa, mgombea urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), amesihi utawala uliopo chini ya Rais Jakaya Kikwete kuwa makini usije ukasababisha vurugu kwa sababu ya kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Akihutubia wananchi wa Misungwi na Magu mkoani Mwanza leo, Lowassa amesema yeye asingependa kuona nchi inachanwa kwa kuwa watu wanataka madaraka ya dola.

“Ninawasihi sana, wawe makini wasije kuleta machafuko kabla na baada ya uchaguzi. Lazima tuendeshe uchaguzi wetu kwa amani na salama,” amesema.

“Haya yanawezekana kwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa yule anayestahili na sio kwa mapenzi ya mtu. Nawaambia sana kwamba ni vizuri wafuate sheria,” amesema.

Lowassa ambaye anagombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alipokuwa Geita, aliwaambia wananchi wajiandae kupokea matokeo yenye matumaini kwao ya kupata mabadiliko ya kweli.

Alipogusia suala la mikataba ya madini mkoani Mwanza, Lowassa alisema akichaguliwa, serikali atakayoiongoza itapitia mikataba yote na kuifumua itakayokuwa haina maslahi na wananchi.

Lowassa amezungumzia suala la serikali kuepuka kuichafua nchi kwa sababu ya uchaguzi wakati kukiwa na msuguano katika hoja ya kutaka wananchi wasikae kwenye maeneo ya vituo vya kupigia kura baada ya kupigakura.

Tume pamoja na Serikali wanasema kila mtu akishapiga kura aondoke maeneo ya vituo ili kuepusha kutokea vurugu na jana Rais Jakaya Kikwete alionya kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayevunja sheria.

Rais Kikwete aliyekuwa akihutubia kilele cha mbio za mwengu wa Uhuru mjini Dodoma jana, alisema serikali isilazimishwe kutenda yasiyopendeza.

Hakueleza yasiyopendeza ni yepi, lakini akionesha hasira usoni, alisema serikali itachukua hatua kali kwa kadri ya uvunjaji sheria utakavyokuwa umefanyika.

Viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA wamekuwa wakishikilia kuwaelekeza wananchi kutoondoka vituoni na kwamba wana haki ya kukaa nje ya mita 200 ili kukabiliana na mbinu chafu za kuiba kura zao.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akiwa Geita jana alisema Rais Kikwete ni vema akaachiwa kumaliza muda wake na aondoke salama kuliko kutoa kauli zinazotishia wananchi wanaodai haki ya kutendewa haki wakati wa uchaguzi.

error: Content is protected !!