July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa ajipalia makaa CCM

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, wakishuhudiwa na Steven Wassira pembeni

Spread the love

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kuzungumza na waandishi wa habari na kumbeza Rais Jakaya Kikwete, kuhusu sera ya kilimo na makada wa CCM, Samuel Sitta na Dk. Harisson Mwakyemba, sasa kibao kimemgeukia, akidaiwa kutapatapa. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Lowassa ambaye alikuwa msaidizi wa Rais Kikwete kwa miaka miwili kama msimamizi wa shughuli za Serikali kabla ya kujiuzulu kwa shinikizo la Bunge mwaka 2008 kwa kashfa ya zabuni tata ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development LLC, alisema serikali alikosea kuanza na kilimo kwanza na kuweka elimu kando.

Pia, Lowassa alijitetea kuhusu Richmond akisema hakula hata senti moja, isipokuwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeongoza Kamati Teule, walipika ripoti ya kashfa hiyo ili kumdhalilisha.

Kama ilivyobashiriwa kuwa, Lowassa ameibua mzozo kwa kukinzana na utaratibu wa CCM unaowataka viongozi kupingana au kukosoana kupitia vikao badala ya kufanya hivyo hadharani, baadhi ya makada wamemjibu wakisema anatapatapa baada ya kuona hana nafasi ya kuteuliwa.

Licha ya Sitta na Mwakyembe kutojitokeza kujibu chochote, lakini baadhi ya watu walio karibu nao, wamelidokeza MwanaHALISIOnline kwamba, wamempuuza Lowassa kwa sababu ukweli wote kuhusu kashfa ya Richmond uko wazi.

“Tumefuatilia kauli ya Lowassa kwa waandishi wa habari, lakini tumeshauri viongozi hawa aliowakejeli wasijibu ili kuvuruga mchakato wa uteuzi kwa sababu baadhi yao wataingia kwenye kinyang’anyiro.

“Lakini kitendo cha kukebehi hata Rais Kikwete ambaye alimwamini na kumpa madaraka makubwa ya uwaziri mkuu kuwa serikali yake ilikosea kuanza na kilimo kwanza badala ya elimu, hii ni dalili tosha kwamba Lowassa anatapatapa baada ya kubaini hana sifa za kuteuliwa kugombea urais,” amesema mmoja wa makada aliyeomba kuhifadhiwa jina lake ili kuepusha mtafaruku ndani ya chama.

Ameongeza kuwa, “anachokifanya sasa ni visasi vya tukose wote. Huyu amekuwa serikalini na hayo anayozungumza ndizo zilikuwa sera za CCM walizozinadi wakati wakisaka urais na badaye akapewa uwaziri mkuu kusimamia hayo”.

Naye mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalah (CCM), ambaye ametangaza nia ya kuomba uteuzi wa kugombea urais, ameandika kupitia mtandao wa kijamii akisema, “kama Kamati ilimuonea Lowassa, basi imuombe radhi na ituombe radhi Watanzania wote”.

Amekwenda mbali zaidi akisema, “kama kweli Lowassa atagombea urais 2015, itakuwaje kwenye mijadala ya uchaguzi na CCM itasimamaje kama itampitisha kuwa mgombea, kumuombea kura wakati ilimuangusha bungeni kutoka kwenye nafasi nyeti ya uwaziri mkuu?

Dk. Kigwangalah amehoji, CCM itatoa majibu gani kuhusu kwa nini ilimuita Lowassa ‘gamba’ na ikatangaza hadharani kuanza mchakato wa kuvua magamba ambao haukukamilika.

“Nilisema jana, Lowassa amefungua pandora box, na kama atatangaza kweli kuwania urais, inabidi haya mambo yawekwe wazi, yamalizwe, maana hauwezi jua ya kesho – ikitokea akawa mgombea wetu, tutaanzia wapi kumnadi na kusema ni mtu safi, muadilifu, anayechukia rushwa na ubadhirifu na kwamba anafaa kuwa Rais, wakati juzi tulisema hafai kuwa waziri mkuu na tukamtoa?

“Nilisema kuwa, CCM haipaswi ku-risk kuteua wagombea wenye mambo mengi ya kutolea maelezo kwa wananchi, ikifanya hivyo itaangushwa asubuhi ya saa nne. Watanzania wa leo siyo wa juzi,” ameandika Kigwangalah kupitia mtandao wa Jamii Forum.

Amefafanua kuwa Lowassa kama amekana kuhusika na Richmond, sasa wanakamati inabidi wamjibu, waweke wazi, na wamjibu kwa uwazi bila kuficha.

“Maana kama alionewa ijulikane na sisi tuliohuzunishwa ama kufurahishwa na Bunge wakati ule tuujue ukweli. Yeye anasema hakuhusika na ndiyo maana Kamati ya Mwakyembe haikuona haja ya kumwita kumhoji. Ukweli tunauhitaji sana leo kuliko jana. Ukweli huu ni haki yetu,” amesema.

error: Content is protected !!