January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa aja na mchaka mchaka wa maendeleo

Waziri Mkuu Aliyejiuzuru na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akitangaza nia ya kuwania Urais 2015 kupitia CCM

Spread the love

EDWARD Lowassa- Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, ametangaza rasmi nia ya kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kugombea urais, huku akijipambanua kwamba anataka kuleta uongozi wa mchaka mchaka wa maendeleo. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Hata hivyo, kinyume na ahadi yake kwa wahariri wa vyombo vya habari alipokutana nao nyumbani kwake mjini Dodoma hivi karibuni, kwamba angefafanua kwa kirefu kuhusu tuhuma dhidi yake juu ya kashfa ya zabuni tata ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, Lowassa hakugusia kabisa suala hilo.

MwanaHALISIOnline limedokezwa na chanzo muhimu kwamba, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na Dk. Harriso Mwakyembe, aliyeongoza Kamati Teule ya Bunge kuhusu kashfa hiyo, wanatarajia kukutana na wahariri kuanika ukweli mzima juu ya sakata hilo baada ya Lowassa kuwatuhumu kwamba walipika ripoti ili kumdhalilisha ajiuzulu uwaziri mkuu.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliofurika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo kutoka mikoa mbalimbali nchini, Lowassa alitumia dakika 30 kusoma hotuba yake, na kuainisha vipaumbele kadhaa akisema “ni maono yangu kuwa siku si nyingi nchi itakuwa kwenye safari ya matumaini”.

Hotuba yake, ilinogeshwa na kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombare-Mwiru, ambaye amemtaka Lowassa kuketi meza moja na wanachama wenzake aliokwaruzana nao ndani ya chama ili kusaka suluhu na kusahau yaliyopita.

Akikatizwa mara kwa mara na kelele za wafuasi wake waliokuwa wakishangilia, Lowassa amesema demokrasia ya mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini inazidi kukua lakini akaeleza kushutushwa namna wanasiasa wanavyozidisha chuki ndani ya vyama.

Amesema kuwa uchumi wa nchi unaendelea kukua huku rasilimali mpya kama gesi na mafuta zikigundulika, japo ukuaji huo hauendani na hali halisi ya maisha ya wananchi, jambo alilodai kuwa safari yake ya matumaini inakusudia kuboresha hayo ili kuwapatia vijana fursa za ajira.

Lowassa alianza kwa kunukua maneno ya hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kwamba watu wanataka mabadiliko. Na kwamba wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM; lakini akatamba kuwa anaamini watajipanga vizuri ndani ya chama na kushinda uchaguzi mkuu.

Amesema kuwa, serikali ya Rais Jakaya Kikwete imefanya mambo mazuri katika kusimamia uchumi wa nchi na kufafanua kuwa mrithi wake ni lazima awe na sifa tano za uongozi.

Amezitaja sifa hizo kuwa ni;- awe na maamuzi magumu, dhabiti na asiyeyumba, mbunifu na mwenye upeo mkubwa, mwenye uongozi shirikishi kwa maendeleo ya Taifa na mwenye kuzingatia muda katika utekelezaji wa majukumu.

Kwa mujibu wa Lowassa, Rais ajaye anapaswa kuwa na uwezo wa serikali yake kukusanya mapato, kubuni sera nzuri za kuwainua watu kiuchumi, kusimamia mali za nchi zisiporwe hovyo na mwenye kuchukia rushwa kwa vitendo.

“CCM hoyeeee…watatuweza? Ameuliza Lowassa na kuongeza kuwa, “nina uwezo wa kuongoza Tanzania”. Lakini wafuasi wake walipoanza kushangilia wakimwita rais…rais…rais, amewaonya akisema “angalieni kushangilia kwenu kusije kumpa Mangula (Philipo), Makamu Mwenyekiti wa CCM, sababu ya kunishughulikia”.

Lowassa ambaye mkutano wake ulihudhuria na wabunge kadhaa wa CCM, mawaziri wa zamani, wenyeviti wa chama wa mikoa kadhaa, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya wananchi, ametamba kuwa anao uwezo wa kuwapa Watanzania uongozi imara.

“Najua kufika Agosti wakati tutakapoanza kampeni tutakuwa na ilani ya chama. Lakini nje ya ilani mgombea naye ana maono yake. Mimi nikichaguliwa nitashughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila, nitasimamia uchumi ili tuondokane na sifa ya kuwa Taifa la watu ombaomba,”amesema na kurejea kauli yake kwamba anachukia umaskini.

Pia aligusia kipaumbele chake alichokipigia kelele muda mrefu cha kujenga upya mfumo wa elimu bora yenye kuzalisha wahitimu wanaouzika katika soko shindanishi la ajira.

Kuhusu Katiba mpya, Lowassa amegusia kwa kifupi, akisema atahakikisha misingi ya kudumisha Muungano imara ulioasisiwa na wazee Julius Nyerere na Abeid Amani Karume inadumishwa.

Pia ameahidi kuboresha huduma za jamii kama upatikanaji wa maji safi na salama, afya bora na mahitaji mengine kwa angalizo kwamba ili kutimiza hayo ni lazima vita ya rushwa ipiganwe kwa vitendo badala ya maneno matupu.

“Mama Lishe, waendesha bodaboda, wamachinga watakuwa marafiki zangu, sitapenda kuona wanasumbuliwa badala yake nitawawekea mazingira bora ya kufanya shughuli zao kwani nao ni Watanzania kama walivyo wengine,”amesema.

Kuhusu hali ya msongamano jijini Dar es Salaam, Lowassa amesema, “Ifikapo Oktoba mwaka huu, kama ule ujenzi wa barabara haujamalizika, nikiingia Ikulu kazi ya kwanza ni kumaliza kabisa tatizo la foleni”.

Kingunge ajifunga

Akiwasalimia wananchi kwa niaba ya wazee na viongozi wastaafu marafiki wa Lowassa, Kingunge Ngombare-Mwiru amesema, “tumeanza safari ya Ikulu. Nawapongeza sana wananchi wa Arusha kwa kazi hii na vilevile nakupongeza Lowassa kwa kutangaza nia. Tumekusanyika hapa watanzania wote”.

Ameongeza kuwa, “hapa tunamzungumza raia. Unapoungumza urais, unazungumza nchi na ukizungumza nchi, unazungumza wananchi. Wazee tunaamini mchakato huu unahusu maslahi ya nchi yetu. Waswahili wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi…mimi naamini Lowassa ndiye Mnyamwezi”.

Kingunge amefafanua kuwa Lowassa akilinganishwa na makada wengine waliotangaza nia ndani ya CCM, anaonekana kuwa na sifa nyingi zaidi kwa vile amelelewa na chama na hivyo ndiye anafaa kuwa Rais na Mwenyekiti wa ajaye wa chama.

“Huwa nawambia viongozi wenzangu kwamba tumeyumbayumba kwa mambo ya hivi karibuni ya CCM isiyo na umoja. Tukiendelea hivi tutasambaratika. Baada ya mikwaruzano yote hadi kufikia hatua ya chama kuwaondolea adhabu mjini Dodoma, sasa tusema yaliyopita si ndele.

“Mkitaka kuganga yajayo lazima kuwe na mchakato wa suluhu (reconciliation). Waliokwaruzana wakutane kwenye kikombe cha chai wayamalize. Na wakitaka kuwaita wazee wapo. Yuko Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa, Pancras Ndejembi na wengine wengi…kazi ya wazee ni kusuluhisha,” amesema.

Kwa mujibu wa kada huyo, wanasiasa hao waliokwaruzana kutokana na makundi yao, wengi ni marafiki wakubwa, hivyo wanapaswa kuitana na kuelezana kwamba “tumekanyagana sasa yaishe…sisi tulifanya hivyo huko nyuma”.

error: Content is protected !!