July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa abeba fomu za urais NEC

Msafara wa Mgombea wa Urais kupitia UKAWA, Edward Lowassa

Spread the love

EDWARD Lowassa tayari amechukua fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za kugombea urais katika kura itakayopigwa Oktoba 25 mwaka huu, siku ya uchaguzi mkuu nchini. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Lowassa ambaye ni waziri mkuu aliyejiuzulu Februari 2008, kuihifadhi Serikali ya CCM iliyokumbwa na kashfa ya mkataba wa Richmond, amechukua fomu hizo mchana leo akifuatana na viongozi wote wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Fomu hizo amezichukua kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CAHDEMA) ambacho kimepewa dhamana na UKAWA kuwakilisha umoja huo katika kampeni ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchukuaji wa fomu, Lowassa alikuwa na mgombea wake mwenza, Juma Duni Haji, mwanasiasa gwiji aliyehamia Chadema akitoka Chama cha Wananchi (CUF) kwa lengo la kutimiza masharti ya UKAWA katika kusimamisha mgombea mmoja.

Duni alikuwa makamu mwenyekiti wa CUF, waziri wa Mawasiliano na Miundombinu na alishateuliwa kugombea kiti cha uwakilishi, jimbo la Bububu, mjini Zanzibar.

Viongozi waliofuatana na msafara wa Lowassa na Duni, ni wenyeviti wa vyama hivyo vinavyoshirikiana akiwemo Dk. Emmanuel Makaidi wa Chama cha National League for Democracy (NLD) na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Kiongozi mwingine ni James Mbatia, ambaye ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi. Wenyeviti wote hao ni wanatambuliwa kama wenyeviti wenza wa UKAWA.

Viongozi wengine ni makatibu wakuu wa vyama hivyo wakiongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Pia alikuwepo Twaha Taslima, aliyeteuliwa jana na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuongoza Kamati ya Muda ya uongozi itakayodumu kwa miezi sita ikifanya kazi za mwenyekiti na makamu ambao wote wamejiuzulu.

Mwenyekiti alikuwa Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu Agosti 5 kwa kudai hawezi kuendelea kushika wadhifa huo kutokana na tofauti na wenzake. Duni alijiuzulu ili kuwezesha kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa.

Msafara wa Lowassa na Duni ukisindikizwa na viongozi wote hao ulianzia Ofisi Kuu za CUF Buguruni, jijini Dar es Salaam ambako tangu alfajiri leo wanachama walikusanyika kusubiri kushuhudia.

Eneo hilo lilikuwa kivutio kwa muda wote mpaka ilipofika saa 5.20 msafara ulipoanza safari ya kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi makao makuu, jengo lililokuwa maskani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, mtaa wa Ohio.

Mkusanyiko mkubwa wa watu Buguruni ulikuwa kama marudio ya jana siku ambayo Lowassa alifika ofisi hizo na kuhutubia Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililokuwa na kikao cha dharura. Lowassa pia alihutubia kwa muda mfupi wananchi waliokuwepo.

UKAWA umeimarika kwa kuingia Lowassa ambaye amefuatwa na makada kadhaa wa CCM wakiwemo waliokuwa wabunge, James Lembeli (Kahama), Dk. Makongoro Mahanga (Segerea), Ester Bulaya (Viti Maalum) na Goodluck ole Medeye (Arumeru Magharibi) ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi.

Wakati watu walijazana Buguruni huku kukiwa na utitiri wa walinzi wa vyama vyote hivyo, shamrashamra zilizidi walipochomoza polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala akiwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU).

Msafara wao uliingia ndani ya uwanja wa ofisi kuu za CUF na kamanda kushuka na kupanda walikokuwa viongozi wakuu ambao walikuwa wakimsubiri Lowassa kuwasili.

Kuliibuka hofu ya namna Fulani, hasa kwa kuwa kabla ya hapo kulishasikika tamko la Kamishna Suleiman Kova wa Kanda Maalum Dar es Salaam, kwamba hawakuruhusu maandamano katika tukio hilo la mgombea wa Chadema kuchukua fomu NEC.

Hata hivyo, baada ya majadiliano marefu, Kamanda wa Ilala aliridhia kuongoza msafara wa viongozi wakuu wa UKAWA kuondoka kwenda makao makuu ya NEC.

Msafara huo ulilazimika kwenda mwendo wa pole kutokana na watu wengi kujitokeza barabarani kila ulipopita ukitumia barabara ya Uhuru kupitia Kariakoo.

error: Content is protected !!