May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu, Zitto ‘kumwaga mboga’ Ulaya

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema

Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wamepanga kuieleza dunia hali ya kisiasa ilivyo Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu anayeishi nchini Ubelgiji pamoja na Zitto aliyeko nchini Tanzania, watatoa tamko hilo leo tarehe 20 Novemba 2020 kupitia mtandao wa Zoom majira ya saa 10:00 Alasiri kwa majira ya Afrika Mashariki.

Lissu aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, alikimbilia nchini Ubelgiji akidai kutishiwa usalama wa maisha yake, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Najma Khamis kuhusu mkutano huo, Zitto na Lissu watajadili na kuchambua mchakato wa uchaguzi huo,  pamoja na majukumu ya Jumuiya za Kimataifa katika maendeleo ya Tanzania.

Uchambuzi huo unakuja katika kipindi ambacho kumeibuka  madai ya kuyumba kwa mahusiano ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa kutokana na uporomokaji wa demokrasia na misingi ya haki za binadamu.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalando

Hadi sasa, kuna taarifa za kwamba Bunge la Jumuiya ya Ulaya (EU), liko njiani kupitisha azimio la kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Tanzania, kwa madai kwamba Taifa hilo limekiuka haki za binadamu katika mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni..

Jana tarehe 19 Novemba 2020, Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la EU inadaiwa kupitisha azimio la kulitaka bunge hilo kushinikiza nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutotoa misaada kwa Tanzania pamoja na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Fununu hizo zinajili siku kadhaa baada ya Chadema na ACT-Wazalendo kuomba jumuiya za kimataifa kuiwekea vikwazo Serikali ya Tanzania kwa madai kwamba, haikutimiza sharti la kuendesha mchakato wa uchaguzi huo katika misingi ya haki na usawa.

Vyama hivyo vilidai mchakato wa uchaguzi huo haukuwa wa haki, kuanzia uteuzi wa wagombea, upigaji kura na utangazaji wa matokeo.

Kufuatia madai hayo, vyama hivyo vilipinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi (ZEC), ambayo yalikipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM)  katika nafasi ya Urais wa Tanzania na Zanzibar.

Lakini pia, matokoe hayo yalikipa ushindi CCM katika uchaguzi wa wabunge, wawakilishi na madiwani.

error: Content is protected !!