December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu: Tudai uwajibikaji ajali ya ndege Bukoba

Spread the love

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Bara, Tundu Lissu amesema kutokana na ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 kwenye Ziwa Victoria Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19, Watanzania wanatakiwa kusimama na kudai uwajibika kwa viongozi wanaohusika na uokozi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Pia amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan awaeleze Watanzania ni lini hao aliowapa dhamana kuhakikisha kuna uokozi, wataondoka madarakani kwa sababu wanaendelea kuchukua fedha za umma na kuishi kwa gharama za umma wakati kwa ajali hiyo ni ushahidi hawafai kuwa kwenye nafasi hizo.

Lissu ametoa kauli hiyo juzi wakati akichangia mjadala kuhusu ajali hiyo ambayo pia ilichukua maisha ya rubani na msaidizi wake.

Ndege ya Precision ikiwa imezama katika ziwa Victoria baada ya kushindwa kutua uwanja wa Ndege wa Bukoba, Kagera

Mjadala huo ambao ulirushwa mubashara kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, pia alieleza kushangazwa na helkopta ambayo ilitumiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuelekea Bukoba, ambayo pia ilitumiwa kupeperusha bango la idadi ya watu Tanzania siku ambayo Rais Samia anatangaza rasmi matokeo ya sensa ya watu ilihali hali helkopta hiyo ni maalumu kwa ajili ya uokozi.

Alisema inafahamika wazi kuwa wakati wa kuruka na kutua kwa ndege ndipo kunapoweza kutokea hatari ndio maana katika viwanja vya ndege maofisa uokozi huwa tayari muda wote pamoja na magari ya kuzima moto.

Kutokana na hali hiyo alieleza kushangazwa na ndege hiyo ambayo ilianguka mita 100 umbali kutoka uwanja wa ndege ulipo lakini hapakuwa na uokozi wala jitihada zilizofanywa na maofisa hao.

Kutokana na kitendo hicho, alisema Watanzania wataendelea kumlaumu Mungu wanapenda kufanya hivyo majanga yakishatokea.

“Mambo ambayo watu wanatakiwa kuwajibika tunamlaumu Mungu na kusema Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe! mwisho wa safari tunagongeshana glasi na maisha yanaendelea.

“Hii habari ya kumlaumu Mungu kila tukio ni mojawapo ya matatizo ambayo tunatakiwa tupambane nayo na tuyakatae, tuwe na utamaduni wa kuyakataa kabisa kama tunataka ku-deal na ajali kama hizi,” alisema.

Alisema kwa rekodi zilizopo, tangu mwaka 2010 kumetokea ajali mbalimbali kubwa nchi kubwa zilizoua mamia ya watu ambazo zingeweza aidha, kuzuiliwa au watu kuokolewa kama kungekuwa na mfumo mzuri wa uokozi.

Alisema mwaka 2011 meli ilizama nje ya kisiwa cha Nungwi Mv Spice Islanders iliua mamia, mwaka 2012 ikazama MV Skagitis wakati ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar na kuua mamia, 2018 meli ya MV Nyerere ikazama ndani ya Ziwa Victoria- Ukerewe ikaua mamia.

Alisema katika matukio yote hayo ni dhahiri kwamba nchi haina utaratibu wowote wa uokozi.

“Kama kuna watu ambao wamepewa dhamana ili wasimamie haya masuala ya majanga ambao waapo chini ya ofisi ya waziri mkuu na mawaziri wengine wanaohusika kama mambo ya ndani wanatakiwa wajiuzulu kwa sababu Serikali imeshindwa kabisa kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa kuzuia au kupunguza ajali,” alisema na kuongeza;

“Yaani ndege inaanguka mita 500 kutoka barabara ya kutua, uwanja wa ndege upo mita 100, jeshi uokozi wapo,  polisi wapo na wote wanaohusika hakuna wanachofanya!.

Alisisitiza kuwa watu hao 19 wamefariki kwa sababu ya uzembe na si kwa sababu Bwana Mungu amewaita.

“Tusipoita majina sahihi, tutaendelea kujificha nyuma ya bwana ametoa, bwana ametwaa. Watu wetu wamekufa sana kwa sababu za kizembe, hatuzungumzii ajali za barabara ambazo watu wanaokufa kila mwaka,” alisema.

Kuhusu helkopta hiyo, Lissu alisema ni maalumu kwa ajili ya operesheni za uokozi.

“Hapo awali tuliona ilikuwa inamu-escot Magufuli kokote alipokuwa anaenda ikiwa kwenye kampeni au safari zake, msafara wa magari 200 unakuwa chini na helkopta juu.

“Sasa hivi inatumika kutuonesha idadi ya watu kama mlivyoona, kuwasafirisha viongozi kama waziri mkuu kwenda kuhudhuria mazishi au kuwaaga waliokufa kwa ajali.

“Siku za nyuma ilikuwa inamtembeza Nape Nnauye kila mahali kagua anuani za makazi, ndege ambayo imenunuliwa kwa fedha nyingi za wananchi na imetengenezwa maalum kwa ajili uokozi, kupeleka waokozi maeneo ya majanga kwa haraka… inatumika kwa sababu ambao hazina uhusiano wowote kabisa na uokozi,” alisema.

Alisema kutokana na tatizo viongozi ambao hawana nia ya kuboresha mifumo ya uokozi, dawa yake sio kuomba Mungu aepushe mbali bali muhimu ni kuchukua hatua za kisiasa.

“Rais atuambie, haya yataisha lini, atuambie hawa aliowapa dhamana kuhakikisha kuna uokozi kuna sababu ya kuendelea kuwa madarakani na kuendelea kuchukua fedha za umma, kuishi kwa gharama za umma wakati kwa ushahidi huu hawafai kuwa kwenye nafasi hizo. Tudai uwajibikaji.

“Nje ya lawama kwa Mwenyezi Mungu tuanze kuulizana hawa tuliowapa dhamana wanatekelezaje majukumu yao, kusema tumuachie Mungu ni kisingizio ambacho kitaendelea kuhakikisha watu wetu wanakufa kwa ajali kama hizo,” alisema Lissu.

Wakati Lissu akisema hayo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa jana aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema “Helkopta zinatengenezwa kwa kazi maalum. Helkopta tulizonazo ni kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo tu. Si helkopta za kuvutia meli au ndege au kitu kizito,” alisema na kuongeza kuwa

“Kukabiliana na athari za majanga zikiwemo ajali ni jukumu la kila mmoja wetu tukiongozwa na wataalamu na mamlaka za uokozi, nawapongeza Wananchi na Viongozi wa Mkoa wa Kagera kwa jitihada walizofanya kukabiliana na madhara ya ajali ya ndege ya Precision”.

error: Content is protected !!