Thursday , 7 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu: Sitaunda Serikali itakayolipa kisasi
Habari za SiasaTangulizi

Lissu: Sitaunda Serikali itakayolipa kisasi

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewasilisha taarifa ya kusudio lake la kutaka kugombea Urais wa Tanzania, kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lissu amechukua hatua hiyo siku kadhaa tangu John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, kuwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, kuwasilisha taarifa zao katika ofisi yake, kuanzia tarehe 3 hadi 15 Juni 2020.

Lissu ametoa taarifa hiyo leo Jumatatu tarehe 8 Juni 2020, wakati akizungumza mubashara na Watanzania akiwa ughaibuni kupitia mtandao ya kijamii.

Makamu mwenyekiti huyo wa Chadema amesema amesukumwa kutaka kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, ili kuinyoosha nchi, katika maeneo ambayo yameyumba kutokana na serikali iliyoko madarakani, kukosa sera na mikakati.

Lissu amesema, endapo atafanikiwa kuwa Rais, ataboresha uchumi wa nchi, mahusiano na jumuiya za kimataifa na nchi marafiki, utawala bora, misingi ya haki za binadamu, demokrasia na mfumo wa vyama vingi.

“Katika kipindi cha miaka mitano itakayoishia Oktoba nchi yetu imetawaliwa na Rais Magufuli na CCM, kwa namna ambayo imeiweka nchi yetu katika mtihani mkubwa wa kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia.

kwa mtihani huo nchi yetu iko njia panda, na kwa vyovyote uchaguzi huu utakuwa wa muhimu katika historia ya nchi yetu,” amesema Lissu.

Lissu amesema uchaguzi wa mwaka huu, utaamua kama Chama cha Mapinduzi (CCM), kitapata fursa ya miaka mitano mingine ya kuendelea kuharibu uchumi wa nchi na kufukarisha wananchi, au mwanzo mpya kwa Tanzania, kujiimarisha kiuchumi.

“Uchaguzi mkuu wa mwaka huu utaamua kama (Rais John) Magufuli atapata fursa ya miaka mitano mingine ya kuendelea kuharibu uchumi na fukarisha wananchi, au kuanza mwanzo mpya wa kiuchumi kwa nchi yetu kwa kumuondoa madarakani,” amesema Lissu.

Lissu amesema, akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha mihimili ya nchi, ikiwemo Bunge na Mahakama, inakuwa huru na kujitegemea kwenye maamuzi yake.

Amesema katika uongozi wake kama atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atavitumia vyombo vya ulinzi na usalama kulinda haki za binadamu, na si katika kukandamiza wapinzani wake, vyombo vya habari na asasi za kiraia.

“Nikiwa Rais, vyombo vya ulinzi na usalama nitavifanya kuwa walinzi wa katiba na haki za binadamu. Serikali yangu haitatumia vyombo hivyo dhidi ya wakosoaji wake, wapinzani au vyombo vya habari huru, “ amesema Lissu.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki ameahidi  akifanikiwa kuwa Rais, Serikali yake itaendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala bora na sheria, inayoendana na Katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa, ambayo Tanzania iliikubali.

Lissu amesema, akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, ataponya majeraha ya wananchi pamoja na kurejesha umoja wa kitaifa, huku akisisitiza kwamba hatalipa kisasi kwa maadui zake.

“Nitajenga umoja wa kitaifa badala ya kulipiza kisasi, serikali yangu itaimarisha umoja wa kitaifa, na kufidia wahanga walioonewa,” amesema Lissu aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Ametumia nafasi hiyo, kusema, ana sifa zote za kuwania Urais kwani katika kipindi chote cha utumishi wake, hajawahi hata siku moja kuitwa, kushtakiwa au kuhukumiwa kwa kosa lolote la kimaadili linaloweza kumkosesha sifa za kuwania nafasi hiyo.

Lissu yuko Ubelgiji tangu tarehe 6 Januari 2018 alikopelekwa akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 mchana wa tarehe 7 Septemba 2017.

Alifikwa na mkasa huo akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge uliokuwa ukiendelea. Tangu wakati huo, Lissu amekuwa nje ya Tanzania mpaka sasa.

Amesema, endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Tanzania kuwaongoza kama Rais, atarudisha hadhi, heshima na madaraka ya Bunge kama mhimili huru wa dola wenye mamlaka yanayolingana na ya Serikali ndani ya mipaka yake iliyowekwa na Katiba.

“Nilikuwa wa kwanza kupigia kelele ukandamizaji mkubwa na dhuluma walizofanyiwa wananchi wa maeneo mbali mbali ya nchi yetu yenye utajiri wa madini,” amesema.

Amesema, nimekuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kabla ya uongozi wangu kukatishwa kikatili na waitwao ‘watu wasiojulikana’ Septemba 7, 2017. Msimamo wangu katika masuala yote muhimu ya nchi yetu na ya watu wetu

unajulikana wazi na wote na haujawahi kutetereka

“Katika utumishi wa kitaaluma na kisiasa wa zaidi ya miaka ishirini, nimetembelea kila mkoa na karibu kila wilaya ya nchi yetu. Kwa sababu hiyo, ninaifahamu Tanzania kwa undani na ninawafahamu Watanzania,” amesema

Lissu amemalizia hotuba yake akimzungumzia Nelson Rolihlahla Mandela, Rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru na ya kidemokrasia alisema yafuatayo siku alipoapishwa Rais wa nchi hiyo tarehe 10 Mei 1994:

“Isijetokea kamwe, kamwe na kamwe kwamba nchi hii nzuri itashuhudia tena ukandamizaji wa mtu mmoja dhidi ya mwenzake na kubebeshwa dharau ya kuwa fungo wa kimataifa.’ Maneno haya yanaihusu nchi yetu kwa sasa,” amesema Lissu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Bashungwa: Katesh kutafanyiwa usafi wa hali ya juu

Spread the loveWAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kuondoa tope...

AfyaHabari za Siasa

RAS Songwe: Tumepigwa… mkurugenzi nakupa siku 21

Spread the loveKATIBU tawala mkoani Songwe, Happines Seneda ametoa siku 21 kwa...

BiasharaTangulizi

Bei ya Dizeli, Petroli yashuka

Spread the loveBEI ya mafuta kwa mwezi Disemba, imeshuka kutokana na kupungua...

Habari za Siasa

Dk. Biteko: Viongozi tuache alama nzuri katika utendaji wetu

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!