MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema, Rais John Pombe Magufuli amebakisha siku 14 kubaki Ikulu, kwa kuwa hatoshinda katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Lissu ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 wakati anazungumza na wananchi wa Kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza, kuhusu changamoto wanazopitia kwenye sekta ya uvuvi katika mkutano wake wa kampeni.
Rais Magufuli anatetea kiti chake cha Urais kwa mara ya pili kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu.
“Magufuli amebakisha wiki mbili Ikulu, tarehe 28 Oktoba 2020 tunawashinda, uchaguzi ukiisha hana kazi,” amesema Lissu.
Akizungumzia ahadi zake, Lissu amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, manyanyaso dhidi ya wananchi hasa wavuvi yatakuwa mwisho.
Amesema, ataunda tume itakayohusisha majaji wa mahakama za juu kuchunguza matukio ya unyanyasaji dhidi ya wavuvi.
“Jambo la kwanza kabisa kuhusiana na hili, kama rais wenu nitaunda tume ya majaji wa mahakama za juu kuchunguza matukio yote ya kuumiza watu, ya kutia watu umasikini ambayo yamefanyika katika mwambao wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Sababu kote nilipopita wavuvi ni kilio kikubwa,”amesema Lissu.
Lissu amesema, lengo la uundwaji wa tume hiyo ni kufahamu watu waliohusika na matukio ya unyanyasaji wa wavuvi, kwa ajili ya kuwachukulia hatua waliohusikanayo.
Pia, Lissu ameahidi kuziboresha sheria za uvuvi, kupanua bandari ya Nansio Ukerewe pamoja na kujenga daraja litakalounganisha kisiwa cha Kisorya mkoani Mara na Ukerewe mkoani Mwanza.
Leave a comment