October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu: Ninamashaka na wanaotaka nirejee

Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki

Spread the love

MWANASIASA mashuhuri nchini na ambunge wa upinzani katika jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, ametilia mashaka “uadilifu” wa watu wanaomng’ang’aniza kurejea nyumbani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja yaliyorushwa kwa njia ya mtandao na chombo kimoja cha habari nchini – Kwanza TV – Lissu alisema, “ninashangaa wanaonitaka nirudi, wakati hata hawaulizi maendeleo yangu!”

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa kuali hiyo, kufuatia swali la mwanaharakati na mmiliki wa mtandao huo, Maria Sarungi, kutaka kujua maoni yake kuhusiana na jambo hilo.

Alisema, “Watu hawa wananitia mashaka. Hawajaniuliza kuhusu maendeleo yangu na gharama za matibabu yangu. Wanang’ang’aniza kurejea nyumbani. Hao wanaopiga kelele kwa kusema arudi arudi nimepona, hakuna hata mmoja aliyeniuliza umetibiwaje? Umeponaje na unaendeleaje?”

Alisema, “kama kurudi, nitarudi. Sijakimbia nchi yangu. Nawapenda sana watu wangu wa Singida Mashariki na viongozi wenzangu wa Chadema na rafiki zangu ambao wamekuwa wananitaka nirudi ili kuja kujenga taifa letu, lakini papo hapo wanafuatilia matibabu yangu. Siyo hawa.”

Kuhusu kauli inayotolewa na baadhi ya watu kwamba amepona, Lissu amewataka watu hao kuwauliza madaktari wake au yeye mwenyewe ili wapate uhakika kuhusu maendeleo ya afya yake.

Akizungumzia kauli ya serikali ya kumtaka arejee nyumbani, ili kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwake, Lissu alisema, “hiyo ni hoja mfu.” Akahoji, “kama ningekufa, uchunguzi usingefanyika?”

Kwa sasa, Lissu yuko nchini Marekani alikokwenda kwa matembezi, wakati akisubiri kufanyiwa operesheni ya 23 katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein, mchini Ubelgiji.

Lissu alikwenda Ubelgiji, tarehe 6 Januari mwaka jana, kufuatia kushambuliwa kwa risasi nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma na wanaoitwa na serikali, “ watu wasiofahamika.”

Shambulio dhidi ya Lissu lilitokea tarehe 7 Septemba 2017, muda mfupi baada ya kushiriki mkutano wa Bunge wa asubuhi na kulihutubia Bunge.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni ameonekana akizunguuka dunia na kufanya mahojiano na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, akiituhumu na kuishutumu Serikali ya Rais John Pombe Magufuli, kuminya uhuru wa kujieleza na kuvunja misingi ya kidemokrasia.

Lissu ameendelea kusimamia hoja kadhaa ikiwa ni pamoja na kitendo cha kuondolewa kwa walinzi katika eneo ambalo shambulio limetokea.

Amesema, si jambo la kawaida kwa eneo hilo linalokaliwa na baadhi ya viongozi wa serikali kukosa walinzi kutokana na kulindwa saa 24.

Amesema, kama viongozi wake wa Chadema wana uwezo wa kuondoa walinzi hadi wa nyumba za viongozi wa serikali, basi Chadema wanahusika, na kama mahasimu wake wa kisiasa wana uwezo huo, basi hao ndio waliotekeleza tukio hilo.

“Kwa nini tunasema haya matukio yanatekelezwa na serikali? Nimesema haya majengo yanalindwa saa 24 mara siku saba kwa wiki mara miaka yote niliyokaa pale. Kuna walinzi wenye silaha, wamekuwapo kwa siku zote. Hakuna siku ambayo pale hapakuwa na walinzi,” ameeleza.

Amesema, “jengo ninalokaa kuna walinzi saa 24 kama mgeni wangu huwezi kuingia hilo jengo bila kukutana na walinzi wangu. Wapo wanaolala getini na kila jengo, siku nimeshambuliwa hawakuwepo. Sikushambuliwa usiku nilishambuliwa saa saba mchana hawakuwepo.”

Lissu amesema, si lazima kubadilisha shift (zamu) kwenye lindo. Wala hakuna uwezekano wa kutokuwa na walinzi kwenye majengo au getini.

Akijibu kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, kuwa  eneo aliloshambuliwa halikuwa na kamera za ulinzi (CCTV) na kwamba yeye (Lissu) anasema uongo, kiongozi huyo wa upinzani ameeleza yafuatayo:

“Nimemsikia Lugola akisema, mahali ninapoishi hakuna CCTV. Mimi nimekaa kwenye hilo jengo tangu mwaka 2010, nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.

“Ninaposema kuna CCTV sizungumzi ya kuambiwa; nazungumzia vitu ambavyo ninavifahamu. Kamera za CCTV ziliwekwa wakati Medard Kaleman (sasa waziri wa nishati) amehamia. Wakati Ngeleja (William Ngeleja, mbunge wa Sengerema) akiwa Waziri wa Nishati na Madini hakukuwa na CCTV. Baadaye akaja Mbunge wa Shinyanga Mjini Masele (Stephen Masele) hakukuwa na CCTV.

“Akaja Medard wakaweka CCTV, ukisimama pale niliposhambuliwa hilo lango la kuingilia la kwanza, unachoona cha kwanza ni CCTV na madirisha, vifaa vyake vingine vilikuwa viko ndani kwa waziri,” amesema.

Jana tarehe 13 Februari 2019 Lugola alisema, Lissu ametelekeza kesi yake, kwanini hataki kurudi nchini? Aache kuwaeleza wazungu kwa sababu wanaopeleleza kesi sio wao.”

error: Content is protected !!