April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu: Niko njiani kurejea nyumbani

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema, ataweza kurejea nyumbani muda wowote kutoka sasa, mara baada ya kushauriana na madaktari wake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika taarifa yake aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii leo tarehe 18 Aprili 2019 na baadaye katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi, Lissu amesema, “nitarejea nchini; sitakubali kukimbia nchi yangu.”

Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, alikuwa akirejea kuwashukuru wananchi – ndani na nje ya nchi – mashirika ya ndani na kimataifa, kwa msaada waliompatia kuanzia matibabu yake, hadi mahitaji yake mengine.

“Nitarejea,” amesema Lissu na kuongeza, “pamoja na kwamba mpaka sasa serikali haijawakamata walionishambulia kwa risasi na jeshi la polisi halijanihakikishia usalama wangu.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi takribani 39 na wanaoitwa watu wasiojulikana tarehe 7 Septemba 2017. Kwa mujibu wake, kati ya risasi hizo, risasi 16 ziliingia kwenye mwili wake.

Amesema, “pamoja na kwamba, waliotaka kuniua mchana kweupe katikati ya mji wa Dodoma, bado wanaitwa ‘watu wasiojulikana; pamoja na kwamba sijahakikishiwa usalama wangu na vyombo vya usalama vya serikali ya John Magufuli, bado sitakubali kuishi uhamishoni.”

Anasema, anaendelea kushauriana na baadhi ya marafiki zake na wadau wengine mbalimbali, wakiwamo madakatari wake, kuhusu tarehe na namna bora ya yeye kurudi nchini.

“Kwa kumalizia, sasa nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa ‘fiti’ kurudi nyumbani. Msiniambie niiseme kwa wakati huu. Tunahitaji kushauriana na wadau mbalimbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani,” ameeleza.

Anasema, “kwa hiyo, wakati muafaka utakapofika, hopefully (nina matumaini) sio mbali sana, nitawaeleza tarehe kamili ya kurudi; na kwa mlioko Dar es Salaam, nitawaomba mniandalie supu ya utumbo wa mbuzi pale Rose Garden kwa Mzee Assey.”

Akizungumzia hali yake ya kiafya, Lissu amesema, kwa sasa majeraha yake yameanza kupona, hivyo anafanya mazoezi ya viungo pamoja na kusubiri kupimwa urefu wa mguu wa kulia.

Anasema, mguu huo ambao ulijeruhiwa vibaya kwa risasi, unahitaji kutengenezwa kiatu maalum kutokana na kuwa mfupi.

“Tarehe 2 ya mwezi huu (Aprili), nilikutana na madaktari wangu kwa appointment (miadi) ya kwanza tangu operesheni za tarehe 20 Februari. Taarifa yao ni kwamba, mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa ‘kiraka’ cha mfupa na kupigwa ‘ribiti’ ya chuma juu kidogo ya goti; na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri,” ameandika katika ujumbe kwake kwa watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumzia malimbikizo ya mshahara wake wa tokea Januari mwaka huu, Lissu amesema, Bunge limelipa malimbikizo hayo.

“Pamoja na kwamba Spika Ndugai amesikika akisema kuwa mambo ya mshahara ni siri ya Bunge na Mbunge husika, na yanatakiwa kujadiliwa ‘chumbani’ na sio ‘sebuleni’, nadhani ni vizuri tukafunga mjadala huu kama ulivyoanza: hadharani.

“Kwa kifupi ni kwamba, Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi Machi waliokuwa wameuzuia kiharamia tu,” ameandika.

Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji, tayari ametangaza kuwa anataka kuwani urais katika uchaguzi mkuu ujao, iwapo atapitishwa na chama chake cha Chadema na kushirikiana na vyama vingine.

error: Content is protected !!