Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu, Membe watwishwa zigo ushirikiano Chadema na ACT-Wazalendo
Habari za SiasaTangulizi

Lissu, Membe watwishwa zigo ushirikiano Chadema na ACT-Wazalendo

Spread the love

HATMA ya kuwapo kwa ushirikiano wa vyama viwili vya siasa nchini Tanzania vya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT- Wazalendo
kuelekea uchaguzi mkuu wa Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 uko njiapanda. Anaripoti Yusuf Katimba, Dar es Salaam  … (endelea).

Ili kutanzia mkwamo au kuhitimishwa kwa mazungumzo kati ya vyama hivyo iko mikononi mwa viongozi wakuu Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, makamu wake na upande mwingine, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na Bernard Membe, Mshauri Mkuu wa chama hicho.

Vyama hivyo, vimekuwa vikihubiri umuhimu wa kushirikiana ili kukabiliana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Pombe Magufuli ambaye tayari mapema leo Alhamisi, amechukua fomu Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutetea nafasi hiyo.

Juzi Jumanne, mkutano mkuu wa Chadema, ulimteua Lissu kuwa mgombea urais sawa na mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo uliofanyika jana Jumatano, ulimteua Membe naye kuwa mgombea urais wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maalim Seif, yeye aliteuliwa na mkutano huo kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Taarifa kutoka ndani ya vyama hivyo zinasema, ili kuokoa majadiliano yanayolenga kushirikiana kwa kuweka mgombea mmoja wa urais, ubunge,uwakilishi na udiwani, ni sharti Lissu na Membe, warudi kwenye meza ili kutafuta mwafaka.

Pia, ugumu wa ushirikiano huo, unachagizwa na wanachama wa Chadema ambao tayari wamekwisha kujipanga kugombea udiwani, uwakilishi na ubunge kuwa tayari kupoteza nafasi hizo kwa baadhi ya majimbo na kata.

Hilo lilijitokeza pia mwaka 2015 kwa baadhi ya washirika wa Ukawa wa Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF kushindwa kukubaliana uamuzi wa viongozi wao wakuu na kusimama kugombea ubunge na udiwani kasha, CCM ikashinda maneno hayo.

“Bila hivyo, hakuna ushirikiano. Bila hivyo, upinzani utaendelea kuwa wasindikizaji, kwa kuwa ndani ya vyama vyetu, wapo watu wanaoangalia ruzuku na maslahi mengine binafsi,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa Chadema ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

“Ukiangalia kwa makini jambo hili, utagundua haraka kuwa hakuna sababu zozote za msingi zinazofanya kutokuwapo ushirikiano mpaka sasa. Lakini kwa kuwa tunaangalia jambo hili kwa uso wa vyama na maslahi binafsi ya baadhi ya watu, ndio maana mazungumzo yanakwama.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kwa hapa ambako vyama vimefikia, ikiwa ni pamoja na mikutano mikuu ya ACT- Wazalendo na Chadema, kupitisha wagombea wao wa urais, “ushirikiano unaweza kufanyika kwa Lissu na Membe, kuketi mezani na kukubaliana kuachiana.”

Vyama vya ACT- Wazalendo na Chadema, vimekuwa kwenye mazungumzo yasiyokwisha tokea Februari 2020 kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kuwapo ushirikiano baina yao katika uchaguzi mkuu.

Jana Jumatano katika mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo, Lissu na Membe walikutana pamoja na kupanda jukwaa kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo ambapo Lissu alikwenda kama mgeni mwaliko.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, “nimefurahi kuwaona wagombea wetu wawili wa urais wakiwa pamoja na kwetu sisi bila kushirikiana itakuwa ni ngumu kuiondoa CCM madarakani na itakuwa rahisi mno kuiondoa CCM madarakani.”

“Tunaendelea kufanya mazungumzo hadi hatua ya mwisho kuhakikisha ni tunashirikiana na kuwa na mgombea mmoja,” alisema Zitto.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Kiongozi huyo alisema “mwenyekiti wetu amefanya kazi kubwa sana ya kuwasilisana na baadhi ya viongozi wa vyama kufanikisha hili. Kwetu sisi ushirikiano na vyama vyengine vya siasa vilivyo makini ni jambo muhimu sana katika kukabiliana na CCM.”

Maalim Seif, akizungumza katika mkutano mkuu wa Chadema aliwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu huo jukumu la kuhakikisha vyama hivyo vinashirikiana liko kwenye mabega yake na mwenyekiti mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo, kusisitiza umuhimu wa vyama kushirikiana na kuongeza, “ACT- Wazalendo, tuko tayari kwa ushirikiano. Nimwombe mwenyekiti mwenzangu (Mbowe), mzigo huu wa ushirikiano upo juu ya bega langu, bega lako.”

“Sisi tukishakubaliana, viongozi wengine hawawezi kukataa. Tuwaunganishe Watanzania. Mpinzani wetu ni CCM peke yake,” amesema

Mbowe mwenyewe aliwataka Chadema kujiandaa na ushirikiano huo kwani kunauwezekano wa kuachiana majimbo na kata akisema “katika kushirikiana, huwezi kupata vyote.”

Lissu: Tunaangalia vikwazo

Lissu akizungumza katika mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo jana Jumatano, aligusia ushirikiano wa vyama hivyo akiwaeleza wajumbe wa mkutano huo “tuko pamoja na tutashirikiana.”

“Lakini katika kushirikiana, kuna mitego mingi kweli kweli, itabidi kama watu wazima wenye busara zao, tutaangalia wapi kwenye ndoana na wapi kuko salama. Lakini nisehe tutashirikiana na tupo pamoja,” alisema.

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema Bara “sisi wa Chadema, hatutafanya jambo lolote la kuhujumu mapinduzi na harakati za miaka mingi za Wazanzibar chini ya uongozi wa Maalim Seif.”

“Sisi wa Chadema na mimi mgombea urais wa Chadema na mgombea wangu mwenza, Salum Mwalimu wa kulainisha ile kama imetumika kunyonga maslahi ya Wazanzibar,” alisema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo aungana na wananchi ujenzi maabara za sekondari

Spread the loveMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za Siasa

CCM apiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye mambo ya kimila

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari za Siasa

Ofisi za mabalozi wa mashina zitumike kuwale vijana kimaadili – Chongolo

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza...

error: Content is protected !!