April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu mbioni kumshitaki Ndugai

Spread the love
TUNDU Lissu, aliyetangazwa na Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, kuvuliwa wadhifa wake wa ubunge katika jimbo la Singida Mashariki, yuko mbioni kufungua shauri mahakamani. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Lissu anatarajiwa kufungua shauri la madai Mahakama kuu ya Dodoma, muda wowote kutoka sasa, kupinga kuvuliwa ubunge wake. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na mwanasiasa huyo, wakiwamo baadhi ya ndugu zake zinasema, kesi hiyo ya kupinga kuvuliwa ubunge, inalenga kuiomba Mahakama kutoa zuio la kufanyika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo, kumtangaza mshindi na kumuapisha kuwa mbunge wa Bunge la Muungano.

Lissu ambaye ni mmoja wa wanasheria mashuhuri nchini, alitangazwa kuvuliwa ubunge tarehe 28 Juni mwaka huu, wakati akiwa matibabu nchini Ubelgiji.Amekuwa nchini humo, tokea mwanzoni mwaka jana, kufuatia kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi, akiwa anahudhuria vikao vya Bunge, tarehe 7 Septemba 2017. Shambulio dhidi yake, lilifanyika nje ya nyumba yake, eneo la Area D, mjini Dodoma. Tangu wakati huo, amefanyiwa oparesheni zaidi ya 19 hadi sasa.

Akitangaza uamuzi huo bungeni, Spika Ndugai, alitoa sababu mbili zilizomfanya kufikia uamuzi huo – kutoonekana bungeni kwa muda mrefu bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Maamuzi ya Spika Ndugai yamekuja miezi sita tokea Lissu kueleza umma kupitia mitandao ya kijamii, kwamba amepata taarifa za mpango wa kumvua ubunge.

Aidha, uamuzi huo umefikiwa katika kipindi ambacho chama chake – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – kimetangaza kufanya mapokezi makubwa ya kumpokea atakaporejea nchini Septemba mwaka huu.

Akitangaza uamuzi huo, Ndugai alisema, “Septemba, 2017 kwa sababu ambazo zinafahamika kwa kila mtu, Mbunge wa Singida Mashariki aliondoka hapa nchini kwa ajili ya matibabu nchini Kenya.

“Kufanya hadithi iwe fupi mtakumbuka zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akionekana kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa  akifanya mihadhara mbalimbali.

“Lakini kwa muda wote huo hajafika bungeni na hajawahi kuleta taarifa yeyote ile kwa Spika kuhusu mahali alipo na anaendeleaje wala hajawahi kuleta taarifa kupitia kwa uongozi wake wa kambi au uongozi wa Bunge,”  Ndugai aliliambia Bunge.

Alisema Katiba ya nchi ipo wazi katika mambo ya aina hiyo  na kwamba baadhi ya wabunge  wameshapata matatizo kutokana na utoro kama huo wa Lissu.

“Wa (utoro) kushindwa hata kuwambia Spika niko mahala fulani naendelea na jambo fulani hivi hakuna chochote, yaani kama kum dis-regard Spika kama hakuna chochote,” alisema Ndugai

Alisema jambo la pili wabunge wanatakiwa kujaza taarifa zenye maelezo ya mali na madeni kama Katiba inavyotaka.

“Tunatakiwa tujaze fomu mbili na nakala inabaki kwa Spika, baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna fomu za Lissu, nilichukua jukumu la kupata uhakika wa jambo hili kwa Kamishna wa Tume ya Maadili na nilijibiwa kwa barua kwamba Lissu hajawasilisha na hawana taarifa zozote,” alisema.

Katika hilo Ndugai alisema kwa maana hiyo Lissu hakuwa amejaa fomu na kwamba katika mazingira hayo kifungu cha 37 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) cha kufanya.

“Sababu ni mbili kutotoa taarifa za mahali alipo na kutotoa tamko la mali na madeni kama ibara ya 71 ( 1g) inavyotaka,”.

“Napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba Jimbo la Singida Mashariki lipo wazi, alijaze kwa mujibu wa sheria zetu” alisema Ndugai

“Narudia kwa kumalizia maana kuna baadhi ya magazeti yataandika spika amfukuza hapana!

“Katiba yetu inasema katika mazingira yale yote mawili ubunge wake utakoma na ataacha kiti chake kwa hiyo unakwenda kinyume, hufukuzwi na yeyote ni kama ‘option’ (chaguo) uliyoichagua mwenyewe wajibu wa Spika ni kumwandia tu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi,” alieleza.

Kabla ya uamuzi alioutangaza jana Ndugai, Lissu ambaye amekuwa mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amejikuta akiingia kwenye mgogoro na Spika Ndugai kutokana na malipo ya matibabu yake na pili kusudio lake la kutaka kumsitishia msharaha.

Kusudio la Ndugai kumfutia Lissu Mshahara, lilitokana na baadhi ya wabunge waliohoji juu ya yeye kuendelea kulipwa mshahara ilihali ahudhurii bungeni badala yake anaitukana Serikali nje ya nchi.

Hata hivyo hoja hiyo ya iliondoka Aprili, baada ya Lissu mwenyewe kutamka kuwa, “Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi Machi waliokuwa wameuzuia kiharamia tu, kwa maoni yangu kilichowafanya wakubali yaishe ni ujasiri wenu, na wa watu wengine wengi, mlioamua kunichangia.”

Ikiwa Lissu ataweza kufungua kesi hiyo na kufanikiwa kuzuia kuapishwa kwa mbunge mpya wa jimbo hilo, huo utakuwa mwanzo mzuri wa kutetea uhuru wa wananchi na haki za kiraia, ameeleza Cecil Mwambe, mbunge wa Ndanda (Chadema).

error: Content is protected !!