January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu, Lema kurejea Tanzania Machi 202

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Gobless Lema, wanatarajia kurudi nchini Tanzania kati ya Machi na Aprili 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akitoa hotuba yake ya kuuaga 2021, kwa njia ya mtandao leo Ijumaa, tarehe 31 Desemba mwaka huu, Lissu amesema hatua hiyo inakuja kufuatia maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema, yaliyowataka kurejea nchini.

Lissu kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji, alikorejea Novemba 2020, baada ya kushiriki Uchaguzi Mkuu, huku Lema akikimbilia nchini Canada, wakidai wamechukua hatua hiyo ili kunusuru maisha yao, baada ya kupata vitisho.

“Katika kikao chake cha tarehe 28 Desemba, Kamati Kuu ilijadili suala la kurudi kwetu kwa kina na kuazimia kwamba mimi na Lema, tuanze kufanya maandalizi ya kurudi nyumbani kati ya mwezi Machi na Aprili ya 2022,” amesema Lissu.

Lissu amesema kuwa, tarehe rasmi ya wao kurejea itatangazwa baadae.

“Kamati Kuu iliazimia kwamba, chama kianze kufanya maandalizi yote ya ujio wetu kwa upande wa Tanzania. Baada ya maandalizi yote kukamilika, tarehe kamili ya kurudi kwetu itatangazwa rasmi kwa wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema,” amesema Lissu.

Godbless Lema

Mwanasiasa huyo amedai kuwa, watakabiliwa na majaribu mengi, lakini hawataka kata tamaa.

“Ninafahamu kwamba, siku zijazo hazitakuwa rahisi. Ninajua tutakabiliwa na majaribu ya kila aina na tutapitishwa katika tanuru kubwa la matatizo na magumu mengi. Licha ya mazingira hayo magumu na mbele ya changamoto kubwa na nyingi zitakazotukabili, hatutainamisha vichwa vyetu na kukata tamaa,” amesema Lissu.

Makamu huyo Mwenyekiti wa Chadema, amesema mwisho wa sintofahamu kuhusu mchakato wa katiba mpya na uhuru wa vyama vya siasa vya upinzani unakaribia.

“Siku hii ya leo inaleta mwisho wa sintofahamu, juu msimamo wa chama chetu kuhusu mchakato wa katiba mpya na juu ya mchakato wa katiba viraka. Inaleta mwisho wa vyama vya siasa vya upinzani wa kweli, kuwa kwenye kifungo haramu cha kutofanya mikutano ya hadhara na maandamano,” amesema Lissu na kuongeza:

“Na inaleta mwisho wa mimi, Lema na wakimbizi wengine kuendelea kuishi uhamishoni. Siku ya leo inaleta mwanzo vile vile, wa harakati mpya za katiba mpya ya wananchi, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba. Inaleta mwanzo mpya kwa siasa za vyama vingi nchini kwetu, baada ya miaka sita ya giza nene.”

Lissu alikwenda nchini Ubelgiji 2017, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana tarehe 7 Septemba mwaka huo, jijini Dodoma.

Julai ya 2020 alirejea kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu, ambapo alikuwa Mgombea Urais wa Chadema, baada ya kushindwa katika uchaguzi huo, miezi kadhaa baadae alirudi Ubelgiji, akidai kutishiwa maisha.

Hata hivyo, vyombo vya dola vilikanusha tuhuma hizo na kumtaka arejee nchini vikimuahidi ulinzi.

error: Content is protected !!