July 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kuwaburuza polisi mahakamani

Spread the love

TUNDU Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ametangaza kuwa jopo la wanasheria wa chama hicho, lipo mbioni kuliburuza kortini Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es kwa kukiuka sheria na Haki za Binadamu, anaandika Charles William.

Polisi inawashikilia vijana, Mussa Sikabwe na Benjamin Nzogu, wakidaiwa kuchapisha maneno ya uchochezi na kurekodi wimbo wa Mwana Cotide, mwimbaji wa chama hicho, unaojulikana kama, ‘dikteta uchwara.’

Vijana hao walikamatwa tangu tarehe 26 ya Agosti mwaka huu, na mpaka sasa hawajafikishwa mahakamani ilihali, sheria za nchi zikilitaka Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani watuhumiwa ndani ndani ya saa 24 baada ya kuwakamata. Hususani kama ni siku za kazi.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma jioni ya leo mara baada ya kutoka Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam, Lissu amesema, “hakuna sababu yoyote halali kisheria kuendelea kuwashikilia vijana hawa katika mahabusu kwa muda wote huu.”

“Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kushikilia mahabusu, ni kazi ya Jeshi la Magereza tena baada ya kupata amri ya Mahakama. Kazi ya Jeshi la Polisi ni kuchunguza au kupeleleza makosa, kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani ili Mahakama iamue kama kweli ni wakosaji au la,” amesisitiza.

Lissu amefafanua kuwa, Jeshi la Polisi linakiuka sheria za nchi kwa kuendelea kuwashikilia vijana hao wawili kwa zaidi ya siku 11 sasa.

“Tunajiandaa kupeleka maombi maalum (habeas corpus) Mahakama Kuu ya Tanzania ili iliamuru Jeshi la Polisi kueleza sababu za kuwashikilia vijana hawa kwa muda wote huu bila kufuata taratibu za kisheria za nchi hii,” amesema Lissu.

Katika hatua nyingine, mwanasheria huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Wilaya ya Ikungi, Singida ameyataka makundi mbalimbali katika jamii kujitokeza na kulaani kitendo hicho, kwani kikivumiliwa kinaweza kujitokeza na kwa watu wengine.

“Juzi ilikuwa Tundu Lissu, jana ilikuwa Freeman Mbowe, leo ni Ben Nzogu na Mussa Sikabwe. Kesho na keshokutwa itakuwa zamu yako au ya ndugu yako. Ukiruhusu mwingine anyongwe haki zake kwasababu haikuhusu, kesho wanyongaji haki watakapokujia wewe hakutakuwa na wa kukusemea,” amesisitiza.

error: Content is protected !!