August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu kuukosa ushahidi wa Kamanda Wambura

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imezitupa hoja za mawakili wa Tundu Lissu, zilizomtaka kamanda Camillus Wambura, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar ea Salaam (ZCO) kufika mahakamani hapo kama shahidi, anaandika Faki Sosi.

Yohana Yongolo Hakimu Mkazi Katika Mahakama hiyo, amesema kuwa hakuna ulazima wa shahidi huyo kutokana na ukweli kuwa, muda wa upande wa utetezi kupeleka mashahidi mahakamani hapo kutofika.

Katika kesi hiyo, Lissu anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kwa kumuita Rais John Magufuli kuwa ni ‘dikteta Uchwara’.

Alidaiwa kutamka maneno hayo mara baada ya kutoka mahakamani katika kesi nyingine inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi kupitia gazeti la MAWIO.

Tarehe 25 Septemba, mwaka huu, Bernard Kongola, Wakili wa Serikali aliieleza mahakama kuwa walikuwa na mashahidi wawili ambao aliwataja kuwa ni (ASP) Kimweli, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Staff Sajenti Ndege.

Hata hivyo, wakili Peter Kibatala, anayeongoza jopo la mawakili wa Lissu aliiomba mahakama iamuru wapewe maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo kabla ya kufanya jambo lolote, jambo ambalo liliibua mvutano wa hoja baada ya kupingwa na upande wa mashtaka.

Wakili Kongola aliieleza mahakama kuwa, mlalamikaji katika kesi hiyo ni Camillus Wambura, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, na kwamba mlalamikaji huyo si miongoni mwa mashahidi wao wanaokusudia kuwaita mahakamani.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai kuwa taarifa ya mlalamikaji huyo ndiyo chanzo cha kesi hiyo na kwamba ni vyema akafika mahakamani kutoa ushahidi kwani maelezo yake ni sehemu muhimu ya kesi.

Uamuzi wa Hakimu uliotolewa mapema leo, umezikataa hoja za mawakili wa utetezi na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mnamo tarehe 5 Oktoba, mwaka huu. Upande wa Jamhuri utaanza kutoa ushahidi mahakamani hapo.

error: Content is protected !!