MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu ametangaza kurejea nchi rasmi tarehe 25, Januari, 2023 ikiwa ni zaidi ya miaka mitano ya kuwa ughaibuni nchini Ubelgiji. Anaripoti Mwandihi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu ametoa taarifa hiyo leo Ijumaa tarehe 13 Januari 2023, katika hotuba yake ya salamu za mwaka mpya 2023 kwa watanzania.
Amesema uamuzi wa kurejea nchini ni baada ya maazimio ya Kamati Kuu ya chama chake kwamba kutokana na mabadiliko ya hali ya kisiasa nchi Lissu na wenzake waliopo ughaibuni warejee nchini.
Wanachama wengine wa Chadema waliopo ughaibuni ni mjumbe wa Kamati Kuu, Godbelss Lema aliyepo
Canada na Ezekiel Wenje. Wote waliondoka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kile walichoeleza kuwa maisha yao yalikuwa hatarini.
“Ukiondoa takribani miezi mitatu ya kipindi cha uchaguzi Mkuu Oktoba 2020 nimeishi uhamishoni kwa zaidi ya mitano kuanzia siku niliyokimbizwa Nairobi Kenya kwa matibabu ya dharura baada ya jaribio la mauji dhidi yangu la tarehe 7 Septemba 2017,” amesema Lissu na kuongeza;
“Hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yangu binafsi na maisha yetu kama chama na kama Taifa.”
Hata hivyo Lissu ameeleza sababu kubwa ya kurejea nyumbani ni kuja kuendeleza kazi kubwa ya kutafuta Katiba Mpya.
“Ninarudi kwaajili ya kazi kubwa iliyopo mbele yetu, kazi ya Katiba Mpya na mwanzo mpya kwa Taifa letu, ninarudi nyumbani kuja kushiriki katika kuandika ukurasa wa kwanza mpya wa kitabu chenye kurasa 365 cha mwaka huu 2023,” amesema.
Leave a comment