Thursday , 2 February 2023
Home Lissu: Kuishi nje kwa kulazimishwa ni ngumu

Lissu: Kuishi nje kwa kulazimishwa ni ngumu

BAADA ya kutua nchini, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema Bara, Tundu Lissu, ameelezea namna ilivyokuwa ngumu kwake kuishi ughaibuni kwa kuhofia usalama wake.  Anaripoti Jonas Mushi,  Dar… (endelea).

Lissu ambaye aliondoka nchini kwa mara ya kwanza Tarehe 7 Septemba 2017 baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi, amesema ilikuwa ngumu kwake,  familia yake,  ndugu, chama na hata Taifa.

Lissu ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, jijini Dar es Salaam,  mara tu baada ya kutua nchini akitokea Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu na baadae kupata hifadhi.

“Naomba mniamini nikiwambieni kuishi nje ya nchi kwa kulazimishwa kwasababu unaogopa utadhuriwa ni kitu kigumu ajabu hii miaka takribani sita saba haijawa rahisi hata kidogo,  kwa mimi binafsi kwa familia yangu kwa andugu zangu kwa chama cha na kwa taifa,” amesema Lissu.

Lissu ambaye alirudi nchini Julai 2020 kwaajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu akiwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema,  amesema amefurahi kurudi nyumbani.

“Niseme nimefurahi sana kurudi nyumbani kwangu na kurudi nyumbani kwetu na niseme sitakuwa nimekosea nikisema na nyinyi mmefurahi pia,” amesema.

Lissu ametumia muda mwingi katika mkutano huo kuelezea umuhimu wa kupata Katiba mpya na kwamba ndiyo kazi aliyoijia.

“Nilipotangaza kuja nilisema nakuja kwaajili ya kazi, kuna kazi yakufanya na hiyo kazi yakufanya ni kazi ngumu kwelikweli,” amesema.

Lissu alirudi Ubelgiji tarehe 10 Novemba 2020 mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi ambapo aliambilia nafasi ya pili nyuma ya mshindani wake mkubwa Rais John Magufuli na kueleza kuhofia kudhuriwa na watu waliotaka kumuua.

error: Content is protected !!