Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Tundu Lissu kuanika wabaya wake
Habari za SiasaTangulizi

Tundu Lissu kuanika wabaya wake

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Spread the love

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, anatarajiwa kuhutubia kupitia mkanda wa video utakaorushwa na vituo mbalimbali vya kimataifa vya televisheni, ndani ya wiki moja kutoka sasa, anaandika Mwandishi Wetu.

Taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa familia ya Lissu zinasema, mwanasiasa huyo shupavu nchini, amepanga kufanya mahojiano na vituo vya televisheni ambayo yatarushwa kupitia mkanda wa video.

Mahojiano kati ya waandishi wa habari wa kimataifa na Lissu yanaratibiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu na utawala bora na vyama vya mawakili ulimwenguni.

Haya yatakuwa mahojiano ya kwanza ya Lissu kurushwa hewani tangu kujeruhiwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” nyumbani kwake mjini Dodoma, tarehe 8 Septemba mwaka huu.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alishambuliwa wakati akirejea kutoka kwenye kikao cha Bunge.

Alikuwa akielekea nyumbani kwa chakula cha mchana na kuandaa maoni ya upinzani kwenye muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali.
Shambulio dhidi ya Lissu limetokea wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”

Taarifa zinasema, katika mahojiano hayo ambayo Lissu atafanya na waandishi wa habari, mwanasiasa huyo amepanga kuanika kilichotokea kabla na baada ya kushambuliwa na wabaya wake.

“Nakuambia hivi, tutarajie mengi sana. Lissu amepanga kuanika kila kitu, kuanzia mipango ya kumshambulia hadi watu waliomshambulia,” ameeleza mmoja wa wanafamilia huyo.

Alipouliza anadhani Lissu atasema nini hasa katika mahojiano yake hayo, ndugu huyo alisema, “hakuna anayejua atakachokisema. Kwa sasa, Lissu anajielewa na anaweza kujisimamia.”

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma na Dar es Salaam, watu waliotaka kuondoa uhai wa Lissu, wanadaiwa kutumia magari mawili – Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.

Dereva wa Lissu anayefahamika kwa jina la Simion Adam, ameliambia gazeti hili, “niliona ile Nissan ambayo ilibeba watu waliompiga risasi Lissu. Tulipoondoka maeneo ya viwanja bunge, lile gari lilitufuata njia nzima hadi nyumbani.”

Simon anasema, siku hiyo ya tukio, alimchukua Lissu nje ya geti la Bunge. Ametaja namba ya gari ambalo lilibeba “wauaji wa Lissu,” kuwa ni Nissan Patrol T 932 AKN.

Anasema, “…kulikuwa na magari mawili, ingawa moja lilionekana kukata njia nyingine, moja lilitufuata hadi nyumbani. Liliingia ndani ya geti la nyumba za Area D, ambako Lissu anaishi. Hilo ndilo lililobeba watu waliomshambulia Lissu kwa risasi.”

MwanaHALISI Online limeelezwa kuwa shambulizi dhidi ya Lissu limesikitisha na kuwakasirisha mamilioni ya watu ndani na nje ya nchi.

Tundu Antipas Lissu ambaye amelazwa kwenye hospitali kuu ya Nairobi nchini Kenya anakopata matibabu ya majeraha ya risasi amewahi kunukuliwa akisema, anawafahamu waliomshambulia.

Akizungumza akiwa kitandani kwake, Lissu amesema, “ninawajua. Nimekutana nao mara kadhaa. Nmewatambua kwa kuwa nilikutana nao Dar es Salaam, wakati wananifuatilia.”

Lissu ambaye ni rais wa chama cha wanasheria nchini, Tanganyika Law Society (TLS), anasema kabla ya urushaji risasi kuanza, alitaka kufungua mlango wa gari lake na kushuka ili aingie ndani ya nyumba yake.

Lakini alisita baada ya kuelezwa na dereva wake kuwa gari lililopo pembeni limeanza kuwafuatilia muda mrefu na hivyo asubiri kwanza.

Anasema, “ninawafahamu. Walianza kutufuatilia kuanzia maeneo ya Tegeta, jijini Dar es Salaam. Pale Dodoma niliwaona kwa jicho langu, nilipobaki kwenye gari kwa zaidi ya dakika 20 nikiangalia nyendo zao.”

“Nilimuona kabisa kabisa. Huyu mtu aliyekuwa anarusha risasi; ninamfahamu. Alikuwa amevaa kapero na miwani myeusi na kizubao… Ni yuleyule niliyekuwa nimekutana naye jijini Dar es Salaam,” anaeleza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!