Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu kuanika mikakati ya Chadema 2022
Habari za SiasaTangulizi

Lissu kuanika mikakati ya Chadema 2022

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

 

MAKAMU mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Tundu Lissu, ataitaja mikakati ya chama hicho kuelekea 2022, kesho tarehe 31 Desemba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 30 Desemba 2021 na Chadema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, Lissu ataitaja mikakati hiyo wakati akitoa salamu za kumaliza 2021 na kulihutubia Taifa, kwa njia ya mtandao. Vyombo vya habari kadhaa ikiwemo MwanaHALISI TV, vitarusha mubashara tukio hilo.

“Tarehe 31 Desemba 2021, saa kumi na mbili jioni, Makamu Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu kulihutubia Taifa, kuufunga mwaka 2021 na kuzungumzia mipango mikakati ya kuingia 2022,” imesema taarifa ya Chadema.

Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani Tanzania, kinaumaliza 2021 kwa kupata misukosuko mbalimbali, ikiwemo mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, kuwa rumande kwa zaidi ya miezi mitano katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Mbali na Mbowe aliyekamatwa na Jeshi la Polisi, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai 2021, jijini Mwanza, washtakiwa wengine katika mashtaka hayo ni, waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Abdillah Ling’wenya.

Wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita ya ugaidi, inayosikilizwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini humo, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Chama hicho pia, kinaufunga mwaka huo pasina kufanya mkutano wake wa Baraza Kuu, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali, kutokana na ukata wa fedha.

Miongoni mwa mambo ambayo yalipangwa kujadiliwa na kutolewa maamuzi na baraza hilo, ni rufaa za waliokuwa makada wake 19, wanaopinga kutimuliwa na Chadema kwa tuhuma za usaliti, baada ya kuapishwa kuwa wabunge viti maalum, kinyume na msimamo wa chama hicho.

Wanachama hao wa Chadema waliotimuliwa ni, Halima Mdee, Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Agnesta Lambart, Ester Bulaya, Esther Matiko, Tunza Malapo, Cecilia Pareso na Asia Mwadini Mohamed.

Wengine ni, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Tarehe 15 Julai mwaka huu, Lissu kupitia mtandao wa Club House, alipoulizwa na wanahabari sababu za rufaa za wanachama hao kukwama kutolewa maamuzi, kitendo kilichotafsirwa kuwanyima haki, alijibu akidai Chadema imekosa hela ya kuitisha kikao cha baraza hilo.

Lissu atalihutubia Taifa akiwa nchini Ubelgiji anakoishi baada ya kukimbia nchi Tanzania na familia yake, akidai hana uhakika wa usalama wa maisha yake baada ya kudai kupokea vitisho vya kuuawa.

Kwa mara ya kwanza, Lissu alienda nchini Ubelgiji Septemba 2017, akitokea jijini Nairobi nchini Kenya, alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, tarehe 7 Septemba 2017, akiwa jijini Dodoma.

Lissu aliishi nchini Ubelgiji kuanzia Septemba 2017 hadi Julai 2020, aliporejea kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2020, ambapo alipitishwa na Chadema, kugombea Urais wa Tanzania na kuambulia nafasi ya pili.

Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kumtangaza mshindi wa kiti hicho kuwa ni John Magufuli, aliyekuwa mgombea wa Chama Tawala Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, Novemba 2020, Lissu alirejea Ubelgiji huku akisindikizwa na maafisa wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania. Aliamua kurejea nchini humo akidai anakwenda kunusuru maisha yake na kujipanga kisiasa.

Hata hivyo, vyombo vya dola Tanzania, vilikanusha madai ya Lissu kutishiwa kuuawa huku Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo, IGP Simon Sirro, akimtaka arejee nchini kwani wako tayari kumpa ulinzi.

1 Comment

  • Asante ndugu lissu lolote usemalo wale watacheka na kukkuona bure kwa sababu wanakutambua hauna uwezo wa kuongea yenye maana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!