August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu hajulikani alipo, Chadema wamsaka

Spread the love

TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki hajulikani alipo. Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Singida wanamsaka, anaandika Josephat Isango.

Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi jana jioni muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara katika Wilaya ya Ikungi, Singida ambapo amelezo yalitolewa kwamba, watu wakalale na kwamba taarifa zaidi zitatolewa leo.

Hata hivyo, viongozi wa Chadema Mkoa wa Singida wanaeleza kuwa, Lissu hayupo polisi na kwamba, hawana maelezo yoyote zaidi kuhusu sehemu aliyopelekwa.

“Tuliambiwa taratibu zote zitaelezwa leo na kwamba, watu wakalale. Kauli hiyo ilitolewa kwa kuwa ilikuwa tayari usiku umeingia,” amesema Shaban Lyimo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida.

Omary Toto, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ikungi amesema, bado hakuna taarifa zinazoonesha wapi alipo Lissu.

“Tumekuwa tukitafuta taarifa kwamba wapi yupo lakini mpaka sasa hakuna taarifa sahihi. Hatujui kama kafichwa hapa hapa Singida ama amepelekwa Dar es Salaam,” amesema Toto.

Taarifa za jana jioni zinaeleza kuwa, Lissu alikamatwa na polisi kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi alipokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam juzi.

Katika viwanja vya Mahakama ya Kisutu Lissu alisema, mwenye mamlaka ya kuzuia mikutano ya kisiasa nchini ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) pekee na si rais wa nchi.

Alisema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa mwongozo huo na si vinginevyo na kwamba, rais hana mamlaka ya kusema au kufanya lolote kuhusu mikutano ya hadhara.

Alitoa kauli hiyo baada ya kutoka kusikiliza kesi anayotuhumiwa kwa uchochezi uliotokana na kauli yake ya ‘Dikteta Uchwara.’

Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema kuwa, mikutano ya kisiasa ifanywe na wabunge na madiwani wa eneo husika.

Kutokana na kauli hiyo Lissu alisema, “ukitaka kujua huu ni dekteta uchurwa, ni pamoja na kauli ya kutaka watu wafanye mikutano kwenye maeneo yao.

“Sheria ya Tanzania inasema kuwa, chama chochote kilichosajiliwa usajili wa kudumu, kina haki ya kufanya mkutano wa hadhara mahala popote nchini isipokua kwenye kambi za majeshi, hasomi sheria, anachofikiria kichwani kwake sio sheria,’’ alisema Lissu.

Akiwa chini ya ulinzi jana Lissu alituma taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii akisema kwamba, aataendelea kudai haki popote walipo.

“Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote walipo,” ni sehemu ya taarifa ya Lissu iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ikungi (Toto) ameuambia mtandao huu kwamba, bado wanaendelea kumtafuta Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema.

error: Content is protected !!