Saturday , 10 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu, Chadema wamsuta Spika Ndugai
Habari za SiasaTangulizi

Lissu, Chadema wamsuta Spika Ndugai

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemjibu Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, kuhusu ya matibabu ya mbunge wake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na chama hicho kwa vyombo vya habari jioni ya leo, tarehe 31 Januari 2019, imemuita spika huyo kuwa “muongo na mbobezi wa upotoshaji.”

“Spika wa Bunge, Job Ndugai amelipotosha Bunge na ameudanganya ulimwengu kuhusu matibabu ya mbunge wetu, Tundu Lissu. Spika wa Bunge, ni kiongozi wa umma. Hivyo ni fedheha kiongozi wa umma kuwa muongo,” imeeleza taarifa hiyo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu, bungeni mjini Dodoma, Spika Ndugai alisema, Bunge limetoa takribani Sh. 270 milioni, kwa ajili ya kuhudumia matibabu ya mwanasiasa huyo.

Kwa takribani mwaka mmoja na nusu sasa, Lissu amekuwa kwenye matibabu yanayotokana na shambulio la lisasi za moto lilitokea nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma.

Katika taarifa yake hiyo, Chadema kinasema, Lissu hajatibiwa na Bunge wala serikali. Bali, ametibiwa na chama chake, michango kutoka kwa wananchi na wanachama wa wengine wa chama hicho, wabunge na madiwani.

“Lissu ametibiwa na chama chake, wanachama mmoja mmoja, mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, Watanzania washio ndani na nje ya nchi na wabunge waliochanga kiasi cha Sh. 43 milioni,” imeeleza taarifa hiyo.

Chadema kinasema, kimelazimika kumjibu Spika Ndugai kwa kuwa bila haya na kwa makusudi ameamua kuliongopea bunge na kuungopea ulimwengu.

“Alichopewa Lissu ni stahiki zake za lazima; na siyo pesa ya matibabu kama alivyoeleza Spika Ndugai. Ni uwongo wa mchana kusema kuwa Lissu amepewa kiasi cha Sh. 270, wakati hicho alichokipata, ni stahiki zake.”

Aidha, taarifa hiyo inasema, “…spika amedai yeye anazo nyaraka za uthibitisho wa malipo ya matibabu ya Lissu. Tunamtaka atoe hizo nyaraka hadharani na siyo kutishia ili kuhalalisha uongo wake.”

Naye Lissu anasema, Bunge la Jamhuri ya Muungano, halijawahi kutoa hata senti tano kugharamia matibabu yake.

Lissu ametoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya Spika Ndugai kusema, Bunge limetoa kiasi cha Sh. 270 milioni kulipia matibabu yake.

Amekiri kulipwa Sh. 43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao kwa matibabu yake. Anasema, kiasi cha fedha kinachotajwa – Sh. 250 milioni – ni mishahara na stahiki zake nyingine, na siyo gharama za matibabu.

Lissu anasema, “njia ya mwongo huwa fupi sana. Mimi sijalipwa hata senti moja ya gharama za matibabu na Bunge. Hata senti moja.

“Shilingi milioni 43 ni michango ya hiari ya wabunge, sio fedha za Bunge kwa ajili ya matibabu yangu.”

Anasema, “nimechangiwa na maelfu ya watu wengine, Watanzania na wasio Watanzania. Hiyo ni michango ya hiari, sio haki ya kisheria ya mbunge anayeumwa.

“Milioni 203.7 zilizobaki ni mishahara na posho za kibunge ambazo kila mbunge analipwa kila mwezi, awe anaumwa au mzima. Hizo nazo sio pesa za matibabu yangu.”

Lissu anasema, “hata Spika Ndugai mwenyewe alipougua na kukaa India kwa zaidi ya miezi sita mwaka 2016, alilipwa mishahara na posho za kibunge, pamoja na pesa ya gharama za matibabu yake.

“Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa kila Mbunge anayeumwa nchini mwetu, isipokuwa kwa Tundu Lissu aliyepigwa risasi 16 akiwa kazini Dodoma, katikati ya vikao vya Bunge.”

Akikazia hoja yake hiyo, Lissu anasema, “hizo milioni 203.7 ni malipo ya jumla kabla ya makato ya kodi ya mapato, makato mengine ya kisheria na makato ya mkopo wa gari.

“Makato haya hufanywa na Bunge moja kwa moja. Ukiondoa makato hayo, malipo yangu halisi hayafiki milioni 6 kwa mwezi.

“Spika Ndugai anajitia aibu yeye mwenyewe na analiaibisha Bunge analoliongoza. Yeye mwenyewe alieleza bungeni mwezi Aprili mwaka jana kwamba Bunge haliwezi kulipia matibabu yangu kwa sababu:

Kwanza, sikupata kibali cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutibiwa nje ya nchi;

Pili, Katibu Mkuu Wizara ya Afya hajatoa kibali cha mimi kutibiwa nje; na

Tatu, Rais Magufuli hajatoa kibali cha kuidhinisha pesa za Bunge kutolewa kwa ajili ya matibabu yangu.

Lakini Lissu anasema, “leo Spika Ndugai anadai nimelipwa pesa ya gharama za matibabu yangu.”

Anahoji, “ni lini alipata vibali hivyo vitatu mpaka wanilipe fedha hizo? Propaganda nyepesi ambazo hazimalizi hata masaa mawili kusambaratika!”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

MichezoTangulizi

Benki ya NBC yakabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu kwa Yanga

Spread the loveMDHAMINI Mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya...

BiasharaTangulizi

TLS wajitosa sakata la ukodishaji wa bandari

Spread the love  CHAMA cha wanasheria Tanzania (TLS), kimejitosa katika sakata la...

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

error: Content is protected !!