Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu azidi kuimarika, kutembea kwa miguu yake kwanukia
Habari za SiasaTangulizi

Lissu azidi kuimarika, kutembea kwa miguu yake kwanukia

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki akiwa na mkewe nchini Ubelgiji akifanya mazoezi
Spread the love

MBUNGE wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, aliyeko kwenye matibabu nchini Ubelgiji, anaendelea kuimarika siku hadi siku. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa za hivi karibuni kabisa kutoka kwa Lissu mwenyewe na watu wanaoshughulikia matibabu yake zinasema, mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini, anatarajiwa kurejea katika hali yake ya kawaida, siyo zaidi ya miezi sita kutoka sasa.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku mbili baada ya kuonekana picha kwenye mitandao ya kijamii, zinazomuonyesha Lissu akiwa kwenye viunga vya Ubelgiji akiwa ameongozana na mkewe, Alicia Magabe.

Katika picha hizo, Lissu anaonekana akitembea kwa kutumia magongo. Kabla ya hatua hiyo, alikuwa akitembea kwa kutumia baiskeli ya miguu mitatu.

Lissu amelazwa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein, kwa takribani miezi miwili sasa, akipatiwa matibabu na madaktari bingwa wa mifupa kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana,” tarehe 7 Septemba mwaka jana.

Kabla ya kupelekwa Ubelgiji, Lissu alipatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Nairobi, anbako madaktari zaidi ya 10 walikuwa wanazunguuka kitanda chake kila siku.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, alishambuliwa kwa risasi za moto majira ya saa saba na nusu mchana, nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma. Alikuwa akirejea nyumbani kutokea bungeni.

Lissu alinusurika kifo, wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”

“Madaktari wanaomhudumia mheshimiwa Lissu, wamethibitisha pasipo na shaka kuwa mgonjwa wetu atapona na kurejea katika hali ya kawaida. Haya wametueleza baada ya kufanyiwa uchunguzi mwingine mkubwa kul Ubelgiji,” ameeleza mmoja wa watu wanaoratibu matibabu ya Lissu nchini Ubelgiji.

Anasema, “hata haya tuliyoyapata ni maendeleo makubwa sana. Lissu amekwenda Ubelgiji akiwa kwenye baiskeli ya miguu mitatu. Leo anaweza kusimama mwenyewe na kutembea kwa msaada wa magongo.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, mara baada ya kumaliza matibabu yake, Lissu atarejea nchini ili kuhudumia wananchi wake wa Singida Mashariki na kuendeleza kile alichokiita, “kuendeleza mapambano ya ukombozi.”

Hata hivyo, mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, amegoma kueleza ni lini hasa mwanasiasa huyo atarejea nchini.

Anasema, “kwa niaba ya wenzangu wote, tunawashukuru sana madaktari wa Ubelgiji, Nairobi Hospital na wale wa Dodoma, waliookoa maisha ya Lissu.”

Maisha ya Lissu, kwa mujibu wake mwenyewe, yalianza kuwa hatarini, siku moja baada ya kumaliza kuhutubia mkutano na waandishi wa habari ulioanika taarifa za kushikiliwa kwa ndege mpya ya serikali aina ya Bombadier Q400.

Ndege hiyo iliyonunuliwa nchini Canada, inashikiliwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd (SCEL), inayodai serikali ya Tanzania dola za Marekani 38.7 milioni sawa na Sh. 87 bilioni.

Mabilioni hayo ya shilingi yanakuja kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake wa ujenzi wa barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo, miaka 20 iliyopita.

Mkataba uliovunjwa na ambao ni chanzo cha deni, ulikuwa Na.10050/98/99 uliopewa jina la “Bagamoyo Project – Dar es Salaam (Wazo Hill).”

Kampuni inasisitiza kwamba ndege haitaachiwa mpaka serikali ilipe kwanza dola milioni 12.5 (sawa na bilioni 27.8) kati ya dola 38.7 inazopaswa kulipa.

Iwapo serikali itashindwa kulipa kiasi hicho, kampuni hiyo itapiga mnada ndege hiyo, imeeleza barua iliyotoka makao makuu ya kampuni hiyo nchini Canada kwenda kwa rais wa Jamhuri, John Magufuli.

MwanaHALISI Online, imeona barua hiyo ambayo imenukuliwa kwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Dk. Augustine Mahiga na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Mugendi Zoka.

Kampuni ya mawakili – Irving Mitchell Kilichman (IMK) – ndiyo ilimwandikia Rais Magufuli, kwa niaba ya kampuni ya SCEL inayoshikilia ndege ya Tanzania.

Ndege hiyo iliyokuwa iwasili nchini Julai mwaka jana, ilikamatwa na kampuni ambayo mkataba wake wa ujenzi wa barabara ulikatishwa wakati Rais Magufuli alipokuwa waziri wa ujenzi – mwaka 2009.

Lissu alieleza kuwa tarehe 10 Desemba, 2009 kampuni ya SCEL ilifungua mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi; na tarehe 10 Juni 2010 mahakama ilitoa tuzo ya dola za Marekani milioni 25 na riba ya asilimia nane (8%) kila mwaka hadi malipo yatakapofanyika.

Katika barua hiyo ya tarehe 4 Agosti 2017, wadai (SCEL) wanarejea mazungumzo kati yao na ujumbe wa serikali ulioshirikisha Dk. Mahiga na Balozi Zoka.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kikao kati ya ujumbe wa serikali na uongozi wa kampuni hiyo kilifanyika tarehe 3 Agosti katika ofisi za kampuni hiyo jijini Montreal, Canada.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Wazanzibar watarajia makubwa kutoka NMB Pesa Akaunti

Spread the loveWateja wapya wa Benki ya NMB wa Zanzibar wanatarajia neema...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kinana aungana na Tale kugawa mitungi ya gesi 800

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda amjibu Mwenyekiti UWT, “wananipa nguvu ya kuwapiga spana”

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemshukia Mwenyekiti wa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madeni ya bilioni 219 yalipwa, wadai wengine waitwa

Spread the loveSERIKALI imesema kuanzia Mei mwaka 2021 hadi sasa imelipa madai...

error: Content is protected !!