January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu awasha moto tena bungeni

Spread the love

TUNDU Lissu-Mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, amewasha upya moto akisema, Rais Jakaya Kikwete ataondoka madarakani bila Katiba mpya aliyowaahidi Watanzania takriban miaka mitano iliyopita. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na msemaji mkuu wa upinzani kwa Wizara ya Katiba na Sheria, ametoa kauli hiyo ikiwa ni wiki moja tangu alipoibua mjadala bungeni akisema Serikali ya CCM ni chovu inapaswa kuondolewa madarakani.

Akisoma maoni ya kambi hiyo kwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2015/16, Lissu amesema “31 Disemba, 2010, Rais Kikwete alilihutubia Taifa na kuwaahidi Watanzania kwamba itakapofika 26 Aprili, 2014 – wakati waGolden Jubilee ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – nchi yetu itapata Katiba Mpya.”

Lissu amesema Golden Jubilee ya Muungano wetu, yaani 26 Aprili, 2014, ilipita bila ya nchi kuwa na Katiba mpya iliyoahidiwa na Rais Kikwete.

“Baadaye tarehe 2 Oktoba ya mwaka huo, ‘Bunge Maalum’ lenye wajumbe wa chama cha waliohusika na EPA, Richmond/Dowans, Tegeta Escrow, Operesheni Tokomeza wafugaji na Operesheni kimbunga dhidi ya Watanzania waishio mipakani, lilipitisha Katiba Inayopendekezwa.

“Hiyo ni baada ya kura iliyopigwa na wafu waliokuwa wametangulia mbele ya haki, mahujaji waliokuwa wanampiga shetani mawe katika Mlima Ararat, Makka nchini Saudi Arabia, wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini India na wajumbe wengine wasiojulikana kwa majina wala walikokuwa wakati wa kura hiyo,”amesema.

Ameongeza kuwa, baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa katika sherehe iliyofanyika hapa Dodoma, Rais Kikwete aliwaahidi Watanzania – kwa mara nyingine tena – kwamba itapigiwa kura ya maoni mnamo 30 Aprili, 2015.

“Ahadi hiyo ilirudiwa rudiwa na kila kiongozi wa CCM na Serikali yake ndani na nje ya Bunge hili tukufu. Hata hivyo, tarehe 30 Aprili ilipita na kura ya maoni iliyoahidiwa na Rais Kikwete haikufanyika.

“Leo ni wiki ya tatu tangu tarehe ya kura ya maoni ipite bila kura hiyo kufanyika na watu wale wale wa chama kile kile kwa maneno yale yale wanatuahidi kwamba kura ya maoni itafanyika katika tarehe ambayo hawaitaji,” amesema.

Lissu ameongeza kuwa, “Wahenga wetu walisema ‘wajinga ndio waliwao.’ Kwa sababu hiyo, Mtanzania yeyote atakayeamini ahadi hewa za watu hawa na chama chao asije akashangaa wala kulalamika atakapoliwa tena.”

Amesisitiza kuwa, “kwa kifupi, hakuna uhakika wowote kwamba kutakuwa na kura ya maoni ili kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa na CCM. Badala yake, uhakika pekee tulio nao ni kuwa Rais Kikwete ataondoka madarakani bila Katiba mpya aliyowaahidi Watanzania.”

Kuhusu fedha za Mahakama na uhuru wa mahakama, Lissu alirejea maoni ya kambi hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/12, kuwa“tatizo kubwa linalozikabili mahakama zetu sio uhaba wa uwezo wa kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili yao, bali ni uhaba wa fedha zenyewe.”

Amesema, katika miaka mitano ya maisha ya Bunge, Serikali hii ya CCM haijawahi kuipatia Mahakama ya Tanzania fedha za kukidhi mahitaji yake kwa mujibu wa vipaumbele vyake.

“Ukweli ni kwamba serikali hii ya CCM haijawahi kukana jambo hili. Wimbo wake ni ule ule wa miaka yote wa ufinyu wa bajeti,” amsema.

Lissu amesema, hali ya miundombinu ya mahakama imekuwa mbaya na ya kusikitisha katika miaka hii mitano ya maisha ya Bunge.

Kuhusu haki za binadamu, amesema kuna kila dalili za kuonyesha kwamba waliyoyapigia kelele badala ya kupungua, yameongezeka. Kwamba, hali ya haki za binadamu katika miaka mitano ya maisha ya Bunge inatisha na imezidi kuwa mbaya.

“Mauaji na mashambulio dhidi ya viongozi wa kidini na waumini wao na sehemu zao za ibada yaliyotokea kati ya mwaka 2012 na 2013 hayajatatuliwa hadi leo. Hakuna mtu yeyote ambaye ameadhibiwa kwa mauaji ya padre mmoja wa Kanisa Katoliki Zanzibar.

“Hakuna aliyeadhibiwa kwa shambulio la risasi na la tindikali dhidi ya mapadre wengine wawili wa kanisa hilo huko huko Zanzibar wala kwa shambulio la tindikali dhidi ya msaidizi wa Mufti wa Zanzibar,”amesema.

Pia ameongeza kuwa,hakuna aliyetiwa hatiani wala kuadhibiwa kwa kuhusika na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki Olasiti- Arusha, lililoua watu watatu na kujeruhi wengine wengi.

“Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au bungeni juu ya wahusika wa mauaji na mashambulio hayo na sababu zake. Mauaji na mashambulio ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine kama madaktari yaliyotokea kati ya 2012 na 2013 hayajatatuliwa pia.

“Maafisa wa Jeshi la Polisi walioamuru mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi hawajachukuliwa hatua yoyote. Badala yake, aliyekuwa kamanda wa polisi hao amepandishwa vyeo na kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi,”amesema Lissu.

error: Content is protected !!