TUNDU Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameahidi kuliboresha Jiji la Dar es Salaam, endapo atashinda Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu ametoa ahadi hiyo leo tarehe 7 Oktoba 2020 alipotembelea maeneo ya Kariakoo jijini humo huku akilakiwa na mamia ya wananchi waliokuwepo kwenye maeneo hayo.
Mwanasiasa huyo amewaomba wakazi wa Dar es Salaam kumchagua ili aliboreshe jiji hilo liwe la kisasa.
“Wakazi wa Dar es Salaam wana kila sababu ya kuniunga mkono sababu tunataka jiji la kisasa, jiji letu linahitaji mabadiliko makubwa, kuna tatizo kidogo kwa mtu asiyetembea, ukiuliza jiji hili lenye watu zaidi ya milioni tano wapi mahali watu wanapumzikia hakuna, nashangaa,” amesema Lissu.

Aidha, Lissu ameahidi kuboresha mfumo wa usafirishaji abiria na bidhaa, kwa kutanua mtandao wa barabara, kujenga njia za reli za juu na chini na usafiri wa majini.
“Nataka tuwe na maeneo maalum kwa ajili ya mwendokasi na iende kila mahali, hauwezi tatua tatizo la usafiri kwa kufanya vitu kidogo kidogo.”

“Unawaonjesha hapa, unawaonjesha pale haiwezekani, lazima tuwe na mfumo wa usafiri kuangalia usafiri wa majini, reli za juu na chini, usafiri wa mabasi, ndiko tunakoelekea,” amesema Lissu.
Lissu anayetumikia adhabu ya kutofanya mikutano ya kampeni kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 3 hadi 9 Oktoba 2020 kw a kosa la kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi, ametembelea Kariakoo majira ya mchana, ambapo amezungumza na wananchi mbalimbali.

Mwanasiasa huyo ametumia usafiri wa Mwendokasi kufika Kariakoo ambapo kila alipopita aliibua shangwe ambapo amefanya manunuzi ya bidhaa kadhaa ikiwemo mchele.
Leave a comment